Home » » Jamii yaaswa kuachana na unywaji pombe uliokithiri.‏

Jamii yaaswa kuachana na unywaji pombe uliokithiri.‏


Na Eleuteri Mangi-MAELEZO

Serikali wilayani Hai imewaasa wananchi kuachana na tabia ya unywaji wa pombe uliokithiri ambao unaathiri nguvu kazi pamoja na maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.

Hayo yamesemwa hivi karibuni na Mkuu wa Wilaya ya Hai Novatus Makunga kufuatia habari iliyochapishwa na gazeti la Habari Leo toleo Na. 02830 la Ijumaa Septemba mwaka huu yenye kichwa cha habari “Ulevi kwa wanafunzi wa Hai wamtisha DC”.

“Si kweli, hakuna kitu kama hicho wala hakuna taarifa za wanafunzi kunywa pombe hizo hali inayopelekea kuwa tishio katika wilaya yetu” alisema Makunga.

Akiongea kwa njia ya simu kutoka wilayani Hai Makunga alisema kuwa alichosema wakati wa mazishi ya aliyewahi kuwa Shehe wa mkoa wa Kilimanjaro Ally Lema alisema wazazi ndio wanaokunywa pombe aina ya gongo na viroba na sio wanafunzi wa shule za msingi wala sekondari.

Akifafanua juu ya suala hilo, Makunga alisema kuwa wazazi pamoja na vijana wengi wanaokaa vijiweni wakiowemo madereva wa “bodaboda” ndio kundi linalosadikiwa kukithiri katika unywaji wa pombe aina ya gongo na viroba ambavyo vinatishia kuathiri mfumo wa uzazi.

DC Makunga aliongeza kuwa pombe hizo ni kali, sio salama na hazina kiwango ndio maana zinapelekea kupunguza nguvu za uzazi ambapo hata Wachungaji wa dini mbalimbali wamesema idadi ya watoto wa ubarikio katika makanisa yao  pia imepungua.

Vilevile wilaya ya nchi nzima inaweza kukosa nguvu kazi kutokana na vijana ambao ndio nguvu kazi ya taifa kupungua au waliopo kutokuwa na nguvu ya kufanya kazi inavyopaswa kutokana na hali yao ya unywaji wa pombe hizo zisizo salama.

Katika kukabiliana na hali hiyo, Makunga alisema kuwa tayari wilaya yake ipo katika hatua za mwisho kukamilisha sheria sheria ndogo ndogo inayopiga marufuku unywaji wa pombe wakati wa saa za kazi wilayani humo.

Makunga alisema kuwa kwa sasa Sheria kuu ya Serikali kuhusu unywaji pombe ndiyo inayotumika ambapo inabainisha kuwa muda wa kunywa pombe siku za kazi yaani Jumatatu hadi Ijumaa ni kuanzia saa 9: 00 mchana hadi saa 4:00 usiku na siku za Jumamosi, Jumapili na siku za siku kuu ni kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa 5:00 usiku ambapo atakayebainika kukiuka utaratibu huo atachukuliwa hatua za kisheria.

Sheria hiyo inataja kuwa anayekunywa pombe saa za kazi atapelekwa mahakamani na kupigwa faini au kifungo cha miezi sita jela au adhabu zote kwa pamoja.
Mwisho.
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa