Home » » MGOGORO UMILIKI MACHIMBO RONGOMA WAANZA KUSIKILIZWA

MGOGORO UMILIKI MACHIMBO RONGOMA WAANZA KUSIKILIZWA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
 
MGOGORO wa umiliki wa machimbo ya moramu na tofali ya Rongoma ambayo yalisababisha vifo vya watu wawili hivi karibuni katika Kijiji cha Masaera, Wilaya ya Moshi vijijini umepelekwa mbele ya Baraza la Ardhi na Nyumba baada ya kudumu kwa zaidi ya miaka 46.
Hivi karibuni, vijana wawili, Adrian Blessing na Shukuru Temu, walifukiwa na kifusi na kufa papo hapo baada ya kuingia kwa kificho katika eneo ambalo lilizuiliwa kufanyika uchongaji wa tofali, hatua iliyofanya serikali kupiga marufuku shughuli yoyote katika eneo hilo kwa muda usiojulikana.
Mgogoro katika eneo hilo ulianza mwaka 1968 ukihusu ndugu wawili, Diana Mosha (44), na mjomba wake Matei Mosha (78-90), ambako inadaiwa kuwa aliyepewa umiliki wa eneo hilo alifukuzwa katika eneo hilo kwa misingi za mila za jamii ya Kichaga kuwa mwanamke hana haki ya kurithi ardhi.
Katika kutafuta haki, Diana alifungua madai baraza la ardhi na nyumba ya Mkoa wa Kilimanjaro dhidi ya mjomba yake, (Matei), ambapo juzi baraza hilo lilikaa chini ya Mwenyekiti wake, Musa Mahelele, kusikiliza rasmi maelezo ya shahidi wa kwanza wa upande wa mdai.
Akitoa ushahidi wake, shahidi wa kwanza katika shauri hilo, Diana Mosha, alilieleza baraza hilo kuwa mwaka 2000 baada ya kukabidhiwa usimamizi wa eneo hilo lenye ukubwa wa mita 200 kwa 200 lililoko ndani ya shamba la familia lenye ukubwa wa eka 16, mdaiwa (Matei) ambaye ni Kaka wa Marehemu Simon alianza kumfukuza katika eneo hilo.
"Mwaka 2000, eneo hili nilikabidhiwa na Marehemu (Simon) Mjomba wangu
ambaye ndiye mlezi wangu, mwaka 2000, baada ya mjomba kufariki alikuja
Kaka yake, Matei Mosha na kunitaka niondoke katika eneo hilo akidai
kuwa yeye ndiye mwenye haki ya kurithi mali ya kaka yake na sio mimi
mwanamke," alieleza Diana.
Akiongozwa na Wakili wake George Kipoko, shahidi huyo alidai baada ya kuona anaelekea kupoteza haki yake, aliamua kukimbilia katika vyombo vya sheria ambapo aliamua kumfungulia mashitaka mjomba wake katika baraza la Ardhi na Nyumba akiamini kuwa huko ndiko usalama wake uliko.
Aidha, Shahidi huyo ambaye ni mmoja kati ya mashahidi wanne wanaotarajiwa kuletwa na upande wa madai, akiwemo Francisca Simon (86), ambaye ni Mjane wa Marehemu Simon Mosha, aliliomba Baraza la Ardhi na Nyumba kufika Rongoma kukagua mipaka ya eneo linalogombaniwa.
Awali, upande wa mdaiwa ukiwakilishwa na Wakili Bahati Chome, ulipinga jaribio la kuwasilishwa kwa Leseni namba 001978NZ, kama sehemu ya kielelezo cha
uhalali wa mlalamikaji, lililowasilishwa mbele ya Baraza hilo kwa madai kwamba haijawahi kuorodheshwa katika orodha ya vielelezo katika shauri hilo.
Akisoma uamuzi wake mdogo, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Musa Mahelele, alisema kuwa kwa kuzingatia mwongozo wa sheria za usuluhishi, inayoelekeza kuwa endapo itaonekana kwamba shauri la awali liliwahi kupokea hicho hicho katika shauri linalofanana, baraza halina budi kulipokea.
Shauri hilo litaendelea kusikilizwa tena Oktoba 16 mwaka huu, saa saba mchana ambako Shahidi Diana Mosha anatarajiwa kuendelea na ushahidi wake.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa