Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Wafugaji wa jamii ya Kimasai kutoka Kenya, wamevamia makazi ya
wakulima wilayani hapa na kuingiza mifugo yao kwenye mashamba hali
inayosababisha uharibifu wa mazao.
Mbunge wa Jimbo la Rombo, Mkoa wa Kilimanjaro,
Joseph Selasini alisema jana kuwa alipofanya ziara ya kushtukiza katika
vijiji vya Mwekiyo na Ngareni alikuta makundi zaidi ya 20 ya ng’ombe na
mbuzi yakiwa katika mashamba ya wakulima.
Selasini alisema hali hiyo ni hatari kwa usalama
wa nchi kutokana na idadi kubwa ya wafugaji kutoka Kenya kuingia nchini
kinyume na taratibu za uhamiaji.
Kutokana na hali hiyo, aliitaka Serikali wilayani
hapa kufanya kikao cha ujirani mwema na Kenya ili kufanya uamuzi wa
kudhibiti uingizwaji wa mifugo hiyo.
“Wafugaji wa Kenya wanaingiza mifugo katika
mashamba ya wakulima wilayani Rombo hasa maeneo ya tambarare hali
inayosababisha ukanda huo kukumbwa na baa la njaa kila mwaka,” alisema
Selasini.
Alisema hali hiyo isipodhibitiwa mapema, inaweza kusababisha migogoro ya ardhi kati ya Kenya na Tanzania.
Mkulima wa Kijiji cha Mwekiyo, James Lyakurwa
alisema wamekuwa wakipeleka malalamiko ya uingizwaji huo holela wa
mifugo katika mashamba yao kwa uongozi wa kijiji lakini hakuna
kinachofanyika.
Naye mfugaji Jonathan Waivera kutoka Kenya
alipoulizwa sababu za kuingiza mifugo yao hapa nchini, alisema
wameuziwa maeneo hayo ya kulisha mifugo.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya hiyo, Elinas
Palangyo alikiri kuwapo kwa wahamiaji hao na kwamba tayari Serikali
imeshavunja mikataba ya mauziano ya mashamba hayo.
Chanzo:Mwananchi
0 comments:
Post a Comment