Home » » KGA WASOGEZA MBELE MGOMO WAO

KGA WASOGEZA MBELE MGOMO WAO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

MGOMO ulioitishwa na chama cha waongoza watalii mkoa wa Kilimajaro (KGA) wa kutaka kusitisha shughuli za kuhudumia watalii katika mlima huo umesogezwa mbele baada ya Serikali kupitia Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) kuomba kukutana na uongozi wa chama hicho Septemba 9 mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari , Rais wa chama hicho, Respicius Baitwa alisema, serikali baada ya kupokea malalamiko yao wameitisha kikao cha haraka kitakachowakutanisha wadau wote wakiwemo waongoza watalii, mawakala wa utalii, KINAPA na TANAPA.
Alisema watu mbali mbali wanaonyesha wasiwasi wao kupitia maoni waliyotoa katika majarida kama All Africa, tovuti mbalimbali ikiwemo ile maarufu ya TripAdvisor ambayo watu takribani millioni 270 wamekuwa wakisoma juu ya uwepo wa mgomo huo.
“Tumepokea barua kutoka Serikali yetu kupitia KINAPA ikituomba kusitisha kusudio la mgomo na kwamba wamepitia malalamiko tuliyotoa, na kulingana na uzito wake watafanya kikao na sisi, kujadili na kutafuta mwafaka ili kuendelea kutoa huduma bora kwa utalii endelevu wa taifa letu.” alisema.
Baitwa alisema kusudio la mgomo huo halikuwalenga watalii bali lilitaka kufanywa kwa ajili ya kuwagomea mawakala wa utalii pamoja na serikali ili waweze kusimamia malipo yao.
Septemba 17, mwaka huu, Wajumbe wa mkutano maalumu wa chama hicho kwa pamoja walitoa maazimio 11 ikiwemo kufanya maandamano yatakayoenda sanjari na mgomo usio na kikomo ili kushinikiza kufanyiwa kazi kwa malalamiko hayo.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa