Home » » ‘KUBADILISHWA MITAALA KUNACHANGIA KUFELI’

‘KUBADILISHWA MITAALA KUNACHANGIA KUFELI’

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

KUBADILISHWA kwa mitaala ya kufundishia shule za Msingi na Sekondari nchini, ni miongoni mwa sababu za wanafunzi kushindwa kufanya vizuri katika mitihani yao ya kuhitimu kutokana na mkanganyiko kwenye mitaala hiyo huku serikali ikikaa kimya, imebainika.
Akizungumza katika mahafali ya 25 ya Shule ya Sekondari Mwanga mkoani Kilimanjaro mwishoni mwa wiki, Katibu wa Utumishi na Utawala wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Ramadhan Dallo, alisema mitaala ya shule imekuwa ikibadilishwa kama njugu hali inayosababisha wanafunzi kufeli.
“Miaka ya nyuma mitaala ilikuwa katika hali nzuri kuliko sasa, hali iliyokuwa ikipandisha ufaulu wa wanafunzi, kwa sasa imekuwa kila mwenye uwezo wa kutoa kitabu cha somo fulani basi tayari utakikuta sokoni… na ikumbukwe kwamba, kila mwanafunzi na akili yake, huyu anaweza kuelewa hivi na yule vile kwenye mada moja,” alisema Dallo.
Dallo, aliongeza kuwa serikali inapaswa kuliangalia hilo, kwani ikilichekea litasababisha ukosefu wa amani na hata usalama wa nchi utakuwa hatarini kutokana na vijana wengi kurandaranda mitaani pasipo kuwa na kazi.
“Tusipojenga mfumo mzuri wa elimu yetu basi tuwe tayari kujenga magereza ya kutosha kwa ajili ya kuwahifadhi vijana wetu wa kike na wa kiume kutokana na ukosefu wa ajira, matumizi ya dawa za kulevya… kwani Wizara ya Mambo ya Ndani haitakaa kimya ikiona uvunjifu wa sheria za nchi, kwanini tufike huko?,” alihoji Katibu huyo.
Hata hivyo, Dallo aliwaponda Walimu wa shule za Msingi na Sekondari hapa nchini wasio na desturi ya kufundisha kile wanachotakiwa kutokana na sababu zisizo na mashiko na kuwataka kukionea huruma kizazi cha sasa na kijacho.
Kwa upande wake, Mkuu wa Sekondari ya Mwanga, Mena Kengera, alisema mitaala inapobadilishwa kila wakati husababisha ufundishaji kuwa mgumu kwa walimu wenyewe na hata kwa wasahishaji wa mitihani hususani ya kitaifa.
“Walimu tunapata tabu sana kumfundisha mwanafunzi kama mitaala itaendelea kubadilishwa bila mpangilio, pia katika usahishaji wa mitihani ya kitaifa inaweza kuleta ugumu wa kuandaa majibu ya swali husika, inawezekana kabisa mwanafunzi alipata lakini alijibu kulingana na kitabu alichosoma,” alisema Kengera.
Risala ya wahitimu iliyosomwa na Emmanuel Bakari na Ruth Shayo, ilikazia zaidi udogo wa maktaba shuleni hapo, ikilinganishwa na idadi ya wanafunzi hali inayowalazimu kupangiwa zamu ya kuingia kila kidato na siku yake.
Wanafunzi 126 wa kidato cha nne walihitimu masomo yao, wakitarajia kuanza mitihani yao ya mwisho mapema mwezi ujao na ikiwa ni maadhimisho ya miaka 27 tangu kuanzishwa shule hiyo.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa