Home » » MLIMA KILIMANJARO WALINDWA KWA MTANDAO

MLIMA KILIMANJARO WALINDWA KWA MTANDAO

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Mlima Kilimanjaro walindwa kwa mtandao
HIFADHI ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro, (Kinapa), imejizatiti kukabiliana na matukio ya moto kwenye maeneo yanayozunguka mlima huo, ambako sasa wanatumia mfumo maalum wa mawasiliano ya ‘internet’ kubaini dalili za moto hatua za awali kabisa.
Hayo yalisemwa juzi na Mhifadhi wa Ikolojia wa hifadhi hiyo, Imani Kikoti, alipokuwa akielezea hatua walizochukua kukabiliana na majanga ya moto ambayo hutokea zaidi wakati wa kiangazi.
Alisema kuwa mfumo huo unaosimamiwa na Wizara ya Maliasili na Utalii, hutoa taarifa za eneo lenye dalili za kushika moto pale tu kunapokuwa na dalili za moshi kwenye maeneo ya mlima Kilimanjaro ambao ni mrefu kuliko yote barani Afrika na moja ya maajabu ya dunia.
“Tunashukuru matukio ya moto yamepungua sana, kwani kwa mwaka huu hakuna kabisa, ila kwa sasa tunafuatilia kwa karibu kupitia mfumo wa ‘internet’ hapa Kinapa na makao makuu ya Wizara ya Maliasili na Utalii… kukiwa na dalili tu tunapata taarifa inatuonyesha na eneo husika, hivyo tunawahi kuudhibiti kabla ya kuleta madhara,” alisema Kikoti.
Alisema kuwa, kwa mujibu wa utafiti wao wamebaini chanzo kikuu cha moto ni ujangili unaosababishwa na watu wanaoingia kwenye hifadhi kwa lengo la kurina asali, ambao hushindwa kudhibiti moto wanaotumia kwa shughuli hiyo.
Kikoti, aliongeza kuwa watu wengine huwinda wanyama kwenye maeneo ya hifadhi jambo ambalo ni kinyume cha sheria, ambao huamua kuwachuna
ngozi na kuwachoma humo humo kisha kuacha mabaki ya moto ambao husambaa kidogo kidogo kabla ya kushika eneo kubwa.

Hata hivyo, alisema kuwa mara chache moto mlima Kilimanjaro kuanzia maeneo ya chini au kusababishwa na wavuta sigara ambao hutupa
ovyo ‘vichungi’ bila kuhakikisha wamevizima, hali inayosababisha moto.

Aidha, alisema kuwa licha ya kuwa na mifumo hiyo ya ufuatiliaji lakini bado wanahitaji ushirikiano zaidi na wananchi wanaoishi maeneo kuzunguka mlima huo, kwa kile alichodai kuwa wao huweza kubaini moto kwa kuwa wanauona mlima huo vizuri.
“Watu wanaoishi maeneo ya Himo au Rombo, huweza kubaini moto mapema kuliko sisi tulio huku juu, kwani mlima huonekana vizuri kwenye maeneo
hayo hivyo ushirikiano wao ni muhimu sana katika kuuhifadhi mlima huu,” alisema Kikoti.

Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro unaotembelewa na watalii wengi kutokana na kuwa na sifa ya kipekee ya kuwa mlima unaosimama pekee duniani (free stand mountain), na moja ya maajabu ya dunia, ambako ina ukubwa wa kilometa za mraba 1,688 kati ya hizo kilometa za mraba 732 ni misitu minene ya asili ambayo husababisha hali ya hewa ya baridi.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa