Home » » MAITI YAKAA MOCHWARI SIKU 34, KISA MGOGORO WA WAZAZI

MAITI YAKAA MOCHWARI SIKU 34, KISA MGOGORO WA WAZAZI

Mgogoro mwingine mkubwa wa kifamilia wa kugombea maiti, umeibuka mjini Moshi na kusababisha mwili wa Rosemary Marandu (38), kuhifadhiwa mochwari kwa siku 34.
Mwili wa marehemu huyo aliyefariki dunia Septemba 4, mwaka huu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC na umekuwa ukilipiwa Sh9,000 kwa siku, hivyo siku 34 gharama yake imefikia Sh306,000.
Tukio hilo limekuwa gumzo mjini Moshi hasa baada ya kutokea siku chache baada ya maiti nyingine ya Steven Assey kufukuliwa kwa amri ya Mahakama na hadi leo ni siku ya 29 bado haijazikwa licha ya mke mdogo wa marehemu, Fortunata Lyimo kupewa haki ya kuzika lakini amekataa akisema ni kinyume cha mila na utamaduni wao kwa mtu kuzikwa mara mbili. Akizungumza jana, mama mzazi wa Rosemary Marandu, Felicia Nkya, alidai kuwa mumewe aitwaye Flavian Marandu ndiye anayeshikilia mwili huo hadi leo.
Marandu ni Diwani wa Kata ya Mrao Keryo kwa tiketi ya CCM na anamiliki vitega uchumi kadhaa vikiwamo viwanda vya kupasua mbao na nyumba za kulala wageni.
“Ukweli ni kwamba tangu amekufa (Marandu) hajatupa taarifa yoyote zaidi ya kunitumia meseji ya simu akiniuliza kama mume wa Rosemary ameniambia kama Rosemary amekufa. Kwa mila na utamaduni wetu, mtu akifa tunakaa pamoja na kupanga mazishi lakini hadi leo hajatuma mtu yeyote kuzungumza na sisi juu ya msiba.”
Felicia alisema walitengana na mumewe huyo mwaka 1982 na mtoto wao huyo amezaa watoto wanane na wanaume tofautitofauti na mumewe aliyemfia, Sigfrid Mlingi naye amezuiwa kumzika.
“Naumia sana napata mateso makubwa ya kiakili na kisaikolojia. Mwezi mzima sasa sijui hatima ya mazishi ya mtoto wangu. Hakuna chakula kinachopita naomba mnisaidie jamani,” alilalamika.
Mama huyo alidai kuwa awali walikwenda kulalamika polisi ambako walishauriwa kufungua shauri mahakamani lakini akadai kwamba hawana nguvu ya kushindana na Marandu.
“Tumeamua kumkabidhi Mungu kwa sababu hatuwezi kushindana naye (Marandu) tukamshinda. Hata kule KCMC anadai kuna kesi mahakamani lakini sisi hatujafungua kesi,” alidai.
Mumewe azungumza
Mlingi alisema ameamua kujiweka kando kushughulikia mazishi ya mkewe baada ya baba mkwe kumtolea lugha isiyofaa.
“Mimi ndiye nilimuuguza hapo Mawenzi mpaka akanifia mikononi mwangu na baada ya kufa nilikwenda Keryo na kuonana na baba yake lakini akanifukuza,” alidai Mlingi.
Alisema awali walikubaliana kufanya maziko Septemba 9, mwaka huu katika Makaburi ya Karanga, Moshi lakini baadaye baba yake akabadilika na kukataa.
“Aliwapigia simu ndugu zangu na kuwatolea lugha isiyofaa na mimi mwenyewe akanitolea kauli za kunidhalilisha na baada ya hapo nikanawa mikono,” alidai Mlingi.
Baada ya kushindwa kuelewana, Mlingi alidai Marandu alituma watu wawili katika Hospitali ya Mawenzi ambao waliouhamisha mwili wa mkewe na kuupeleka kuuhifadhi KCMC.
Alisema hajui kama mkewe ambaye amezaa naye watoto watatu alishazikwa au la na kwamba kwa yote yaliyotokea amemwachia Mungu.
Baba aeleza sababu za kutozika
Hata hivyo, akizungumza kwa simu kutoka Iringa, Marandu alikanusha kuwa kiini cha kutozikwa kwa mtoto wake huyo akisema anasita kuzika bila kupata ridhaa ya mama yake.
“Hao (mama na mume) wananizushia maneno mengi sana, lakini ukweli ni kwamba tangu amekufa hawajataka kuja tuzungumze pamoja na kupanga mazishi” alidai Marandu.
Marandu alidai kuwa mzazi mwenzake huyo alikwenda mbali na kumshtaki polisi ambako rafiki yake wa karibu ambaye ndiye aliyekwenda kuuhifadhi mwili KCMC kwa niaba yake, alikamatwa na kuhojiwa.
“Hivi leo katika mazingira hayo nikizika halafu akatokea mume wake akanishtaki akidai haki ya kuzika si maiti itafukuliwa? Ndiyo maana nataka waje tukae tuzungumze tupange mazishi pamoja”.
Marandu alisema ili kuepusha kadhia, ameona ni busara utata huo ukatatuliwa kwanza na njia pekee ni pande zote zinazohusika kushiriki katika kupanga mazishi hayo.
Lakini badala yake, Marandu alidai kuwa mama wa marehemu anashirikiana na baadhi ya ndugu kutoa matangazo ya uongo redioni kuwa mazishi yamepangwa kufanyika keshokutwa wilayani Rombo.
“Mimi sijawahi kutoa tangazo redioni linalohusu mazishi lakini ni wao wamekwenda redioni na kutoa tangazo hilo,” alidai Marandu na kusema atarejea Moshi kesho kushughulikia suala hilo
Chanzo:Mwananchi

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa