Home » » KAMPUNI YAHUSISHWA VIBALI VYA UTOROSHAJI WANYAMA

KAMPUNI YAHUSISHWA VIBALI VYA UTOROSHAJI WANYAMA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

KAMPUNI ya HAM Marketing and Gumbo Enterprise ya jijini Arusha imetajwa kuhusika katika uombaji wa vibali vya kukamata wanyama hai
154, wakiwemo Twiga wanne waliotoroshwa kwenda uarabuni kupitia uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Shahidi wa 30 wa upande wa Jamhuri, Godson Massawe, aliyekuwa dereva wa mshitakiwa namba moja, Kamran Ahmed, raia wa Pakistani, aliieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Moshi juzi namna ambavyo kampuni hiyo ya Kitanzania ilivyoomba vibali katika ofisi ya Maliasili ya Sietist Arusha.
Akitoa ushahidi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Simon Kobelo, Massawe ameieleza kuwa alikutana na Kamran Ahmed, mwaka 2007, wakati huo akifanya shughuli zake za udereva wa magari madogo ya kusafirisha abiria na kwamba baada ya kuwa marafiki, Mpakistani huyo alimtaka awe dereva wake binafsi ombi ambalo aliliridhia.
Massawe alidai kuwa mwezi mmoja baada ya kuanza kazi ya kumuendesha Kamran, mshitakiwa wa pili, Hawa Mang’unyuka alifika ofisini kwao na baada ya mazungumzo marefu na bosi wake, aliitwa na kupewa taarifa za kubadilishiwa kazi.
Alidai kuwa baada ya hapo waliondoka na kwenda moja kwa moja hadi katika ofisi ya Maliasili ambako Hawa aliwatambulisha kama washirika wake katika biashara ya kukamata na kusafirisha wanyama na kuongeza kuwa yeye alipewa jukumu la kupeleka maombi ya vibali vya ukamataji katika ofisi hiyo kwa niaba ya Kampuni ya HAM Marketing and Gumbo Enterprise inayomilikiwa na mshitakiwa namba mbili.
Akiongozwa na Wakili wa Serikali, Evetha Mushi, shahidi huyo aliieleza mahakama hiyo kuwa katika vibali hivyo vilivyokuwa ni kwa ajili ya biashara ya wanyama hai kwenda nje ya nchi na ambavyo vilikuwa vikilipiwa kulikuwa na majina ya wanyama hai waliotakiwa kukamatwa ambao ni Twiga, Kudu, Swala,  Nyumbu na baadhi ya Ndege.
Katika kesi hiyo, Mpakistani, Kamran Ahmed pamoja na Watanzania watatu, Hawa Mang’unyuka, Martin Kimathi na Michael Mrutu, wanakabiliwa na mashitaka ya kusafirisha kinyume cha sheria wanyamapori hai 152 wakiwamo Twiga wanne, kwenda Jiji la Doha nchini Qatar.
Kamran na wenzake wanadaiwa kuwatorosha Twiga hao na wanyama wengine wenye thamani ya sh. milioni 170.5 kwa kutumia ndege kubwa la Jeshi la nchi ya Qatar, Novemba 26, Mwaka 2010, kupitia KIA, kinyume cha kifungu namba 84(1) cha sheria namba 5 ya uhifadhi wa Wanyamapori ya mwaka 2009. Kesi hiyo itaendelea tena kwa ajili ya kusikilizwa Novemba 24, 25, 26, 27, na 28, mwaka huu.
Chanzo:Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa