ZAIDI ya wanachama 100 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kijiji cha Sanya Hoye wilayani Siha, Kilimanjaro, wametangaza kutaka kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), huku wakimtaka mbunge wa jimbo hilo, Aggrey Mwanri, kwenda kupokea kadi zao wanazojiandaa kuzirudisha.
Uamuzi wa kukihama CCM unatokana na madai ya kuchakachuliwa kwa mgombea wao katika kura za maoni, kutotumika kwa kadi halisi za CCM na badala yake kutumia risiti za malipo ya ada za uanachama huku viongozi wa kata na wilaya wakimpitisha mgombea wanayemhitaji wao.
Wakizungumza kwa niaba ya wenzao, wanachama Denis Bantazary na Magdalena Kimathi, walisema ni vyema mbunge wao ambaye pia ni Naibu Waziri Tamisemi, aje
apokee kadi hizo kabla hawajaamua kuzipeleka CHADEMA.
Katika malalamiko yao ya msingi, wanachama hao walidai katika kura za maoni za awali za CCM kijijini hapo, mgombea waliyemchagua Juma Salum, alipata kura 76 huku akifuatiwa na Josephat Tesha (31), na Moses Munuo (23).
Walisema katika mazingira yasiyoeleweka, walielezwa uchaguzi huo ni batili na kulazimika kurudia siku iliyofuatia, ambako Munuo alipata kura 120, akifuatiwa na Salum kura 79 huku Tesha akijitoa.
Bantazary, alisema CCM haitaki demokrasia ifuate mkondo wake bali wanataka kufuatwa kwa matakwa ya viongozi wa Kata na Wilaya, jambo ambalo hawawezi kulivumilia.
"Tunataka tumkabidhi Mwanri kadi zote maana ni mbunge wetu na tunamwamini, lakini hili linalofanywa na chama chake hatukubaliani nalo na tunafanya hivi ili ajue kwamba tumekerwa na hili," alisema Bantazary.
Aidha, wanachama hao walitaka viongozi wa CCM Wilaya kufanya marekebisho ya kasoro hizo kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa Desemba 14 mwaka huu, vinginevyo suala hilo litakigharimu chama hicho.
Akijibu tuhuma za uchakachuaji wa kura hizo, msimamizi wa uchaguzi huo ambaye pia ni Katibu wa Umoja wa Wanawake (UWT), Kata ya Sanya mjini, Sara Nasari, alisema uchaguzi huo ulikuwa halali na zilitumika kadi za CCM na kwamba, kinacholalamikiwa ni chuki binafsi.
Alisema uchaguzi ulilazimika kurudiwa baada ya mgombea Munuo kukata rufaa kwamba, kura za duru ya kwanza zilianza kuhesabiwa kabla ya muda wa kupiga kura kumalizika na kusababisha baadhi ya wanachama kushindwa kupiga kura.
Alipohojiwa kuhusu yanayolalamikiwa katika kura za maoni, Katibu wa CCM Wilaya ya Siha, Allan Kingazi, alimuhoji mwandishi wa habari hizi kuwa; Kama kura zimepigwa na mshindi amepatikana unataka uandikaje, kisha kukata simu.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment