Home » » WAZIRI MGIMWA ATAKA WAONGOZA WATALII WAWE NA MIKATABA HALALI

WAZIRI MGIMWA ATAKA WAONGOZA WATALII WAWE NA MIKATABA HALALI

NAIBU Waziri wa Maliasili na Utaliii, Mahmoud Mgimwa, amewataka waongoza watalii hapa nchini kuhakikisha kuwa wana mikataba halali ya kazi na wamiliki wa kampuni wanayofanyia kazi ili kuepuka kunyonywa haki zao.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa mwaka wa Chama cha Waongoza Watalii Mlima Kilimanjaro (KGA), kilichofanyika mjini hapa, Mwenyekiti wa chama hicho, Respicius Baitwa, alimwelezea waziri huyo kuwa pamoja na ugumu wa kazi yao, baadhi ya wamiliki wa kampuni za utalii wamekuwa wakiwanyonya haki zao.
“Nimesikiliza risala yenu kwa makini sana, changamoto kubwa mliyoeleza ni maslahi duni kutokana na kulipwa ujira mdogo na waajiri wenu ambao ni wamiliki wa makampuni ya utalii, hivyo nawasihi muwe makini hasa katika suala la mikataba yenu ya kazi ili serikali iweze kutetea haki zenu, maana ninyi ni mabalozi wa utalii,” alisema Naibu Waziri Mgimwa.
Waziri huyo, aliwaahidi waongoza watalii hao kuwa, atakutana na Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Utalii nchini (Tato), pamoja na Chama cha Wamiliki wa Kampuni ya Utalii Kilimanjaro (KIATO), ili kuona namna ya kulinda maslahi ya waongoza watalii hao.
Mgimwa, alifafanua kuwa hifadhi ya mlima Kilimanjaro ndio hifadhi ambayo inaiingizia serikali mapato makubwa ikilinganishwa na hifadhi nyingine, hivyo kuwataka waongoza watalii hao kufanya kazi zao kwa umakini, uadilifu na nidhamu ya hali ya juu, kwani kinyume chake watalikosesha taifa mapato makubwa yatokanayo na utalii.
Pia, waziri huyo aliwataka wanachama wa KGA kuuendeleza umoja wao ili waweze kusaidiana katika kutatua changamoto zinazowakabili ikiwemo ukosefu wa vifaa maalumu vya kupandia mlima Kilimanjaro.
Kwa upande wake, Mhifadhi mkuu wa Kinapa, Erasto Lufungulo, alisema waongoza watalii wamekuwa sehemu kubwa katika kuyatunza mazingira ya hifadhi ya mlima huo.
Kwa upande wao, waongoza watalii waliokuwepo mkutanoni hapo walisema yao ya moyoni kuwa serikali ili kurupuka kutaja viwango vya malipo kwa siku, kwani kuna kampuni nyingine hazizingatii kiwango cha dola kati ya 15 hadi 20 kutokana na ukweli kwamba, zinalipa zaidi ya kiwango hicho huku wakiongeza kuwa wanamshangaa Naibu Waziri kutaka kukaa meza moja na kampuni hizo ambako awali hawakuzifuata.
Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa