WIZARA ya Maliasili na Utalii, imekubali kukaa meza moja na Chama cha Wamiliki wa Makampuni ya Kitalii Nchini (TATO) ili kutafuta
ufumbuzi wa mvutano wa kimasilahi uliomudu kwa muda mrefu kati ya pande hizo.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa, aliyasema hayo katika Mkutano Mkuu wa tatu wa chama cha waongoza watalii mkoani Kilimanjaro (KGA), na kueleza kuwa ili kuhakikisha mvutano huo unafikia kikomo kwa ajili ya ustawi wa sekta ya utalii nchini.
"Sisi kama Wizara tutawaita TATO na KGA kwasababu sisi kama
Wizara tuliwahi kutamka awali kwamba waongoza watalii walipwe dola za kimarekani 20 na wengine dola 15, lakini tulikwenda haraka sasa tunataka tuwaite wenzetu tuzungumze nao," alisema Mgimwa.
Mgimwa alisema kutokana na umuhimu wa waongoza watalii katika ustawi
wa utalii nchini, Serikali itahakikisha inapambana kuboresha hali yao
kiuchumi ambapo aliagiza uongozi wa Hifadhi za Taifa (TANAPA) pamoja
na Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) kuhakikisha inaandaa kikao
cha wadau wa utalii kujadili swala la Maslahi ya Waongoza watalii
kabla ya mwisho wa mwaka huu.
Aidha Mgimwa aliitaka KGA, kuhakikisha wanachama wake
wanakuwa na mikataba na makampuni wanayofanya nayo kazi kama njia ya
kupunguza manung’unuki ya kila mara.
Awali akisoma Risala ya waongoza watalii, Mwenyekiti wa KGA,
Respicious Baitwa, aliiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kutoa tamko
rasmi juu ya viwango vya malipo kwa waongoza watalii na kushirikiana nao katika kuwaendeleza kitaaluma.
Chanzo:Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment