Home » » NGAWAIYA AUKWAA UONGOZI MOSHI

NGAWAIYA AUKWAA UONGOZI MOSHI

ALIYEKUWA Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi ya Chama cha Mapinduzi(CCM), mkoani Kilimanjaro kwa miaka 10, Sammy Ngassa, ameangushwa na Thomas Ngawaiya katika uchaguzi wa jumuiya hiyo uliomalizika juzi.

Uchaguzi huo ulifanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa jengo la CCM Mkoa. Thomas Ngawaiya kwa muda mrefu alikuwa mpinzani mkubwa wa CCM alipokuwa NCCR- Mageuzi na TLP kabla ya kuhamia CCM katika miaka ya hivi karibuni; alitwaa ushindi kwa kupata kura 270 dhidi ya mpizani wake.

Ushindi wa Ngawaiya ulikuwa na upinzani mkali kiasi cha kuwalazimu wajumbe wa mkutano huo kurudia kupiga kura ili kumpata mshindi baada ya duru la kwanza kumalizika bila kumpata mshindi hadi Ngawaiya kupata kura 197 huku Ngassa akipata kura 130 na Festo Kilawe kutoka Rombo akiambulia kura 121.

Kutokana na hali hiyo upigaji kura kwa nafasi Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ukarudiwa na Ngawaiya kuibuka na ushindi wa kura 270 dhidi ya kura 170 alizopata Ngassa huku kura nne zikiharibika.

Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi, Ngawaiya, alitamba kuwa CCM itashinda kama ‘umeme’ katika jimbo la Moshi Mjini, katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2010 huku akitaka kuvunjwa kwa makundi ndani ya chama hicho.

Naye Mbunge wa Moshi Vijijini na Naibu Waziri na Viwanda, Biashara na Masoko, Dk.Cyril Chami, alishinda katika mazingira tata kwenye nafasi ya Mjumbe wa Baraza Kuu la Wazazi Taifa.

Washindani wa Dk.Chami katika nafasi hiyo akiwamo Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Same, Augustine Kessy na Diwani wa Kata ya Rau, Christopher Lyimo, walijitoa dakika za majeruhi na kuzua minong’ono kutoka kwa wajumbe.

Baada ya wapinzani hao wa Chami, kujitoa msimamizi msaidizi wa uchaguzi huo na katibu wa UVCCM mkoa wa Kilimanjaro, Neema Adam, alimtangaza Chami, mshindi kwa kura 387 huku kura 59 zikiwa zimeharibika.

Naye mwandishi wa siku nyingi, Josephine Sanga juzi alishinda nafasi ya uwakilishi katika Jumuiya ya wanawake ( UWT) kwa kupata kura 246 na kuwaacha wapinzani wawili kwa mbali.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Manispaa ya Moshi, kwa vipindi viwili, Joseph Masika na Diwani wa Kata ya Rau, Christopher Lyimo, waliangushwa vibaya kwenye nafasi ya ujumbe wa Baraza Kuu la Wazazi Mkoa na nafasi hiyo kuchukuliwa na Abdallah Mtwenge aliyepata kura 212.

 Chanzo;Tanzania Daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa