Home » » 16 KIZIMBANI VURUGU ZA WAFUGAJI SIHA

16 KIZIMBANI VURUGU ZA WAFUGAJI SIHA

 Shamba la Ndarakwai lililoteketezwa kwa moto
WAKAZI 16 wa Kijiji cha Miti Mirefu na Sanya Juu wilayani Siha, Kilimanjaro wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Hai wakikabiliwa na makosa ya kuvamia shamba la mwekezaji, kampuni ya Tanganyika Film and Safari Tawi la Ndarakwai na kuchoma moto mali zenye zaidi ya thamani ya sh bilioni 1.7
Wakisomewa mashtaka mbele ya Hakimu Mfawidhi, Denis Mpelembwa, Mwendesha Mashtaka Roymax Membe, alidai kuwa watuhumiwa hao wote kwa pamoja walitenda  makosa hayo kwa kuvamia shamba la Ndarakwai linalomikiwa na mwekezaji Peter Jones, Novemba 14 mwaka huu.
Membe, alidai kuwa watuhumiwa hao walitenda kosa la kwanza la kuingia ndani ya shamba la Ndarakwai na kuchoma magari sita ya kambi ya utalii ya Ndarakwai yenye thamani ya sh milioni 450 kinyume na kifungu cha 299 cha makosa ya jinai cha 2002.
Alidai kosa la pili watuhumiwa hao waliharibu mali za mwekezaji huyo kwa makusudi,  ambazo zina thamani ya zaidi ya sh bilioni 1 na kosa la tatu walichoma mali za mwekezaji huyo zenye thamani ya sh milioni 210 kinyume na kifungu cha 326 (i) cha makosa ya jinai cha mwaka 2002.
Awataja watuhumiwa hao kuwa ni Matey Hilita (42), Julias Daudi (45), Elipokea Sefano (42), Andrea Elias (67), Alex Filipo (30), Victor Joakimu (32), na Dickson Mallya (38), wote wakazi wa Miti Mirefu.
Wengine ni Dickson Kweka (62), Emmanuel Isaya (17), wakazi wa Sanya Juu, Erick Wilson (27), Rahel Paulo (26), Bibiana Charles (36), Hellen Stepahano (39), Hellen Daudi (26), na Monika Rongai (42), wakazi wa Miti Mirefu.
Mwendesha Mashtaka huyo, aliieleza mahakama hiyo kuwa upelelezi bado haujakamilika na kuiomba mahakama kutotoa dhamana kutokana na thamani halisi ya vitu vilivyoharibu kutokujulikana.
Watuhumiwa wote wamekana mashtaka hayo na Hakimu Mpelembwa alikubali ombi la Mwendesha Mashtaka huyo na kutoa siku saba awakilishe thamani halisi ya uharibifu huo. Kesi hiyo imeaharishwa hadi Desemba 2 mwaka huu itakapotajwa tena.
 Chanzo;Tanzania daima
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa