Home » » ADAIWA KUUA NDUGU AKIMTUHUMU KUIBA KUNI

ADAIWA KUUA NDUGU AKIMTUHUMU KUIBA KUNI

MKAZI wa Kijiji cha Mboni, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro, aliyefahamika kwa jina la Harold Kiwelu au Mzalendo (36), ameuawa kikatili na mtu anayedaiwa kuwa ndugu yake kwa madai ya kuiba mzigo wa kuni wenye thamani ya sh. 5,000.

Wakizungumza na Majira kwa nyakati tofauti, ndugu wa marehemu wakiwemo wazazi wake, walisema tukio hilo lilitokea Desemba 22,2014.

Baba wa Marehemu, Naftali Kiwelu, alisema siku ya tukio, saa 11:45 alfajiri, alipigiwa simu na mtu aitwaye Shahidi Kiwelu akimweleza kuwa amempata mwizi wake wa kuni na tayari amemkamata na kumfunga kamba ili akatoe taarifa katika vyombo vya sheria hivyo aende kumuona.

Alisema baada ya kwenda eneo la tukio, alimkuta mwanaye akiwa amelazwa kando ya barabara akiwa tayari amefariki dunia ambapo mtuhumiwa (Kiwelu) ambaye anamwita marehemu baba mdogo, alikuwa akiendelea na biashara dukani kwake.

"Nilimuuliza mjukuu wa kaka yangu nini kimetokea, naye alinijibu walitaka kumpeleka katika vyombo vya sheria wakati tayari alikuwa amefariki dunia...niliamua kupiga simu kwa viongozi wa Serikali ya kijiji ambao walifika eneo la tukio na kutoa taarifa polisi," alisema.

Aliviomba vyombo vya dola kumsaka mtuhumiwa ambaye inadaiwa ametoroka na kumfungulia mashtaka hali ambayo itasaidia kukomesha vitendo vya mauaji ambayo yanaendelea kushika kasi katika jamii.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Bi. Elimiko Mmbando, alisema siku ya tukio saa 8 usiku, alipigiwa simu na mpangaji katika nyumba yake akimweleza kuwa amemkamata mwizi wa kuni zake.

"Nilitoka nyumbani kwangu na baada ya kufika eneo la tukio nilimkuta mtuhumiwa akiwa amemshika marehemu ambaye alikuwa akivuja damu puani...baada ya kumsogelea nilibaini ni kijana wa mtaani na kumtaka mtuhumiwa asimpige tena.

"Nilizungumza na marehemu ili kujua kama kweli kahusika na wizi wa kuni, niliwapigia simu majirani wachache ambao walifika eneo la tukio tukalijadili suala hilo na baadaye nilimtaka mtuhumiwa ampigie simu baba mzazi wa kijana huyo nami nikaondoka kurudi nyumbani," alisema.Majira lilimtafuta Ofisa Mtendani wa kijiji hicho, Bw. Edward Matemba, ambaye alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kudai kuwa, mtuhumiwa alitoroka siku ya tukio na hadi sasa anatafutwa na vyombo vya dola.

"Nilifika katika eneo la tukio na kumkuta marehemu kalazwa kando ya barabara, tulimkamata mtuhumiwa, kumfunga kamba na kumtaka Mgambo aitwaye Goodluck kumchunga aweze kuwasubiri polisi, wakati tunaendelea kuchukua maelezo ya wazazi na majirani, mtuhumiwa alikimbia.

"Mgambo aliyekuwa akimlinda alikuwa akimfuata kwa nyuma ili kumkimbiza ambaye naye hadi sasa hajulikani alipo...kijiji kimesikitishwa na msiba huu, marehemu alikuwa akifanya shughuli ndogondogo na useremala," alisema.

Aliongeza kuwa, ofisi yake haikuwahi kupata taarifa za marehemu kujihusisha na vitendo vya wizi ambapo hadi sasa Jeshi la Polisi linawashikilia baadhi ya watu.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Geofrey Kamwela, alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, alisema yuko nje ya ofisi na kumtaka mwandishi amtafute leo.

Kwa mujibu wa ndugu wa marehemu, taarifa ya uchunguzi wa daktari aliyemfanyia vipimo, inasema ndugu yao alifariki kutokana na kipigo alichokipata sehemu mbalimbali za mwili.

Chanzo:Majira

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa