Home » » HIACE YAUA SITA K’NJARO

HIACE YAUA SITA K’NJARO

WATU sita wamefariki dunia na wengine kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria aina ya Toyota Hiace namba T 118 ABP, kugongana na gari jingine aina ya Coaster yenye namba T 925 BUX katika eneo la Uchira, Wilaya ya Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Taarifa zilizopatikana eneo la tukio, zinasema ajali hiyo ilitokea baada ya Coaster kupasuka tairi la mbele na kuigonga Hiace ubavuni; hivyo kusababisha lipoteze mwelekeo na kupinduka.

Mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema Coaster ilikuwa ikitokea Moshi mjini kwenda Mwanga na ilipofika eneo la Karimsingi Uchira, ilipasuka tairi ya mbele na kuigonga Hiace iliyokuwa ikitokea Mwanga kwenda Moshi mjini.

Akizungumzia ajali hiyo kwa njia ya simu, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Moshi ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Hai, Novatus Makunga, alisema idadi kamili ya watu waliokufa na majeruhi haijafahamika vizuri; bali taarifa za awali zinasema waliokufa ni sita.

“Ajali imetokea leo (jana), saa 6:45 mchana, chanzo chake hakijafahamika lakini uchunguzi zaidi unaendelea ili kupata taarifa sahihi za tukio hilo.

Alisema miili ya marehemu imehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC na majeruhi wamelazwa katika hospitali hiyo wakiendelea na matibabu.

Kamanda wa Polisi mkoani humo, Geofrey Kamwela, amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema akipata taarifa kamili atazitoa kwa waandishi wa habari leo.

Chanzo:Majira

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa