Mbunge wa Arusha mjini (Chadema) Godbless Lema amesema atamtoa
kwa mabavu bungeni Waziri wa nishati na madini,Profesa Sospetre Muhongo
katika kikao kijacho cha Bunge endapo atakuwa hajaondolewa kwenye nafasi
hiyo.
Mkakati huo wa Lema umeungwa mkono na Mbunge wa
Arumeru Mashariki (Chadema), Joshua Nassari ambaye pia amepanga kumtoa
bungeni kwa nguvu, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew
Chenge.
“Keshokutwa nakwenda bungeni kufanya kazi moja tu,
nikimkuta Muhongo bungeni ndipo nitafukuzwa ubunge moja kwa moja,”
alisema Lema huku akishangiliwa wananchi na kuongeza; “Nikimkuta Muhongo
bungeni na Chenge bado ni viongozi mimi nitakwenda kumshika Muhongo
nimtoe bungeni kwa sababu Katiba inaruhusu kila raia kukemea uovu.”
Profesa Muhongo na Chenge ni miongoni mwa viongozi
ambao Bunge liliazimia wawajibishwe na mamlaka zao kutokana na kashfa
ya uchotwaji mamilioni ya fedha katika Akaunti ya Tegeta Escrow.
Hata hivyo, wakati Rais Jakaya Kikwete
akilihutubia Taifa, Desemba 22 mwaka jana kupitia wazee wa Dar es
Salaam, alitangaza kumweka kiporo Profesa Muhongo kwa siku mbili au
tatu, ahadi ambayo haijatekelezwa.
Tayari Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji
Frederick Werema anayehusishwa na sakata hilo alishatangaza kujiuzulu na
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka
akifutwa kazi.
Kauli ya Lema
Akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika juzi
katika Viwanja vya Relini mjini Moshi, Lema alisema Januari 27 mwaka huu
ataingia bungeni akiwa na lengo moja tu la kumtoa kwa mabavu, Profesa
Muhongo.
“Eti Tibaijuka kapewa tu bilioni moja kaondoka, waziri mwenye dhamana hajavuliwa nyadhifa. Rais Kikwete vipi?” alihoji.
Lema alidai kwamba sakata hilo, katibu binafsi wa
Rais ambaye hata hivyo hakumtaja kwa jina, ndiye aliyeandika barua
kuruhusu fedha za escrow zitoke lakini hadi sasa yuko salama na
hajawajibishwa.
Pia, alihoji sababu za Jaji Werema kutofikishwa
mahakamani wakati ndiye aliyefanya makosa katika kutoa ushauri uliozaa
sakata la escrow badala yake watu wadogo ndiyo wanashtakiwa.
“Leo tunaona watu wanapelekwa mahakamani, Rais Kikwete nikuulize
swali, ulisema siyo fedha za Serikali ni za watu binafsi mbona mnashika
watu mnawapeleka mahakamani?” alihoji Lema.
Alisema Sh306 bilioni za escrow zingeweza kujenga
nyumba 15,000 za walimu, kununua mashine 300 za CT -Scan na kujenga
barabara ya lami yenye urefu wa kilomita 600 lakini zimeliwa na
wachache.
Kauli ya Nassari
Akihutubia, Nassari alisema yupo bega kwa bega na
Lema katika kumtoa kwa nguvu bungeni Profesa Muhongo, huku akisema Bunge
lijalo litawaka moto.
“Lema umesema hapa ukimkuta Muhongo bungeni uko tayari kuvuliwa ubunge na mimi si mdogo wako? Tuko pamoja,” alisema na kuongeza:
“Nitamwambia Lema kaba kule na wewe Sugu (Joseph
Mbilinyi, Mbunge wa Mbeya Mjini) kaba kule halafu mimi narukia pale
kwenye Siwa, tunaondoa Siwa tutamfuata Muhongo alipo,” alisema.
Nassari aliwataka wananchi wa Moshi kufuatilia
kikao hicho cha Bunge na akisema haiwezekani maazimio ya Bunge
yasitekelezwe kwa ukamilifu wake na kwa wakati.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment