Wananchi wa Jimbo la Vunjo mkoani Kilimanjaro wamechanga
Sh200,000 za nauli ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba ili aweze kufika jimboni humo kutoa somo la Katiba.
Fedha hizo zilitolewa juzi na kukabidhiwa kwa
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia wakati akihutubia mikutano ya
hadhara kwa nyakati tofauti katika miji ya Himo na Moshi Mjini kwa lengo
la kuwashukuru wananchi kwa kuwaamini wagombea wa Ukawa na kuwapa
ushindi katika Uchaguzi wa Serikali za Mitaa.
Akizungumza wakati wa makabidhiano ya fedha hizo,
Katibu wa Umoja wa Wanawake wa NCCR-Mageuzi, Getrude Pwila alisema kama
hazitatosha kwa nauli ya Jaji Warioba, wako tayari kuchangishana
kuongeza.
“Tunataka tuelimishwe hii Katiba Inayopendekezwa
kwa sababu hatuko tayari kuipigia kura kwa sababu hatuielewi, hatujaiona
wala kuisoma na kuielewa,” alisema Pwila kwa niaba ya wananchi wa jimbo
hilo.
Katibu huyo, alimwomba Mbatia ambaye pia ni Mbunge
wa Kuteuliwa, amwombe Jaji Warioba kwenda katika jimbo hilo kuendesha
kongamano kama alivyofanya katika miji ya Mwanza na Dar es Salaam na wao
wako tayari kumgharimia.
“Leo tunayo nusu ya nauli (Sh200,000) akikubali
tuko tayari kuchangia na kujazia Sh200,000 nyingine na tunakukabidhi
shati la kitenge kama alilokuwa anavaa Mandela (Nelson) ili
ukamkabidhi,” alisema.
Pwila alisema wananchi wa Vunjo wanamchukulia Jaji Warioba kama Mandela wa Tanzania, ndiyo maana wamempatia shati hilo.
Jaji Warioba alipoulizwa kuhusu maombi hayo, alisema hajayapokea na hajui lolote.
Katika mkutano huo, pia wananchi walimkabidhi
Mbatia suti mpya ambayo wanataka aivae atakapokwenda bungeni kuapishwa
akiwa mbunge wa jimbo hilo.
Mbatia awasha moto
Kwa upande wake, Mbatia ambaye pia ni Mwenyekiti
mwenza wa Ukawa, alimtaka Rais Jakaya Kikwete kutekeleza masuala
aliyokubaliana na viongozi wa vyama vya siasa kupitia Kituo cha
Demokrasia Tanzania (TCD) mwaka jana.
Mbatia alisema moja ya makubaliano hayo yalikuwa ni kufanya
mabadiliko ya Katiba ya sasa ili kuruhusu kuwapo kwa tume huru ya
uchaguzi ili Uchaguzi Mkuu wa Oktoba uwe wa huru na wa haki.
Vilevile, mabadiliko hayo yangeruhusu kuwapo kwa
mgombea binafsi, matokeo ya uchaguzi wa rais kuhojiwa mahakamani,
mshindi wa urais kupata zaidi ya asilimia 50 ya kura na kuahirisha kura
ya maoni hadi mwaka 2016.
Akihutubia mkutano katika Mji mdogo wa Himo,
Mbatia alisema mwaka huu hawako tayari kuona Uchaguzi Mkuu unavurugwa na
wasimamizi wanaopokea maelekezo ya Serikali. “Ninamwomba Rais asimamie
maridhiano haya kwa masilahi mapana kwake na kwa nchi yetu kabla miezi
yake hii minane aliyobakia nayo haijawa michungu kwake,” alisema.
Mbatia alisema makubaliano hayo yalikuwa ni ya utu
na kwamba kwa utafiti alioufanya anaona giza mbele na hakuna uwezekano
wa kupitishwa kwa Katiba Inayopendekezwa kwa vile haina maridhiano.
“Naomba kama inawezekana wote tuseme Katiba Inayopendekezwa hapana,
hapana, hapana! Badala ya kulumbana tuangalie kesho, hatutaki uchaguzi
mkuu wa kumwaga damu,” alisisitiza Mbatia.
Mwanasiasa huyo aliyetangaza nia ya kuwania ubunge
katika Jimbo la Vunjo, aliishauri Serikali iwakukutanishe haraka
viongozi wa vyama vya siasa kutafuta maridhiano ya kitaifa kwa kuwa
Ukawa hawako tayari kuigeuza nchi kuwa ya machafuko.
ChanzoMwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment