Licha ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni
na Michezo kuahidi kuwasaidia wasani katika kudhibiti wizi wa kazi zao,
wadau wa sanaa nchini wamesema kuwa hawaridhishwi na adhabu
zinazochukuliwa na vyombo vyenye mamlaka ya kulinda na kutetea haki za
wasanii nchini.
Kutokana na kukithiri kwa wizi na uchakachuaji wa
kazi za wasanii, wadau hao wameitaka Serikali kuingilia kati kwa
kuwachukulia hatua zinazostahili kisheria wale wote watakaobainika
kuhujumu wasanii.
Mbali na kutoridhishwa na hatua zinazochukuliwa
pia wamewataka wasanii kufanya kazi zao kwa weledi na ubunifu kwa
kuingia darasani na kuacha tabia ya kulipua kwa lengo la kufanya
biashara.
“Sanaa ni kazi kama kazi nyingine, kazi ya msanii
inahitajika kuheshimiwa na kulindwa kwa mujibu wa sheria, kanuni na
taratibu zake na kwa wale wote watakaobainika kuwa wanaihujumu
wadhibitiwe na kuwajibishwa,” anasema Edwin Semzaba.
Semzaba ni Mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam (UDSM), alieleza hayo wakati alipokuwa akitoa mafunzo kwa vijana
toka vikundi vitatu vya sanaa ya maigizo vya Malezi Youth Theatre,
Lumumba na Parapanda.
Anasema kwa hapa nchini bado mchango wa taaluma
katika sanaa ya maonyesho siyo nzuri, hasa ikizingatiwa kuwa watu wengi
wanaamini kuwa ni kipaji hata bila ya kuwa na elimu kitu ambacho siyo
kweli.
“Kuna tofauti kubwa kati ya mtu mwenye kipaji na
mtu aliyepata mafunzo, kwa kuwa aliyepata mafunzo ana wigo mpana wa
kufanya shughuli zake tena kwa ubora kuliko yule mwenye kipaji lakini
hana mafunzo,” alibainisha Semzaba.
Semzaba ambaye ni mwandishi wa vitabu, mwigizaji
wa Sanaa za Maigizo na Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi Vitabu nchini
(Uwavita) anasema sanaa ya maigizo ni ngumu na yenye gharama,
ikilinganishwa na sanaa za filamu licha ya kuwa inafanya vizuri.
Alisisitiza kuwa iwapo Serikali ingeweka sera
madhubuti ambayo itasaidia kulinda na kudhibiti wizi na uchakachuaji wa
kazi za wasanii nchini ingeweza kuwainua wao kiuchumi pamoja na pato la
taifa kama ilivyo kwenye nchi za wenzetu.
Lakini kutokana na kuwapo kwa ukosefu wa sera hiyo
madhubuti wasanii wamekuwa wakilia na kuingia hasara kutokana na kazi
zao kuibwa na kuchakachuliwa kila kukicha.
Semzaba ambaye ni mtunzi wa kitabu cha Ngoswe
Penzi Kitovu cha Uzembe, anasema ili mtu awe msanii mzuri katika tasnia
ya Sanaa ambayo inakuwa kwa kasi ni lazima apitie mafunzo ili aweze
kufanya kazi zake kwa ufanisi na weledi.
Anasema moja kati ya vitu vinavyosababisha kazi
nyingi za wasanii kushindwa kufanya vizuri katika soko la kimataifa, ni
kutokana na kufanya kazi zao chini ya kiwango kwa kujikita zaidi kwenye
biashara (masilahi zaidi) bila ya kuzingatia maudhui ili kazi iwe na
ubora unaohitajika.
Vinavyodumaza sanaa
Anasema moja kati ya vitu vinavyosababisha Sanaa
ya maigizo kushindwa kufanya vizuri ni kukua kwa teknolojia pia sanaa ya
maigizo ni ngumu na ina gharama kubwa ikilinganishwa na sanaa ya
nyingine.
Bila kufafanua anasema licha ya teknolojia kuwa
nzuri katika ulimwengu wa sasa, lakini kukua kwa teknolojia hiyo
kumechangia sanaa ya maigizo ishindwe kufanya vizuri katika soko.
“Kukua kwa teknolojia kumesababisha Sanaa ya
maigizo kushindwa kufanya vizuri na hii inatokana na ukweli kwamba sanaa
ya maigizo ni ngumu na ina gharama kuliko sanaa nyingine, lakini ndiyo
sanaa pekee ambayo mtu akiamua kuifanya anaifanya kwa weledi na ustadi
wa juu kwani mtu hawezi kufanya sanaa ya maigizo kama hajapitia
darasani,” anafafanua.
Anasema mbali na Sanaa ya maigizo kuwa na gharama
kubwa pia mapato yanayotokana na Sanaa za maonyesho ni madogo na hiyo
inatokana na watu wanaukuja kutazama au kuangalia maonyesho ya sanaa za
maigizo kuwa wachache tofauti na maonyesho mengine.
Nini kifanyike
Anasema ili kukuza tasnia ya sanaa ya maigizo
nchini, ni wakati wa kuboresha Sanaa hiyo kuanzia shule za msingi ili
kuwa na wasanii wenye utaalamu na hivyo kukuza vipaja na kuongeza ajira
kwa vijana.
Anabainisha kuwa tasnia hiyo inatakiwa iunde sera
ambayo itatumika shuleni ili kuibua vipaji kupitia somo la sanaa, kwani
uwezo wa kufundisha masomo hayo upo na walimu wa masomo ya sanaa ni
wengi ikilinganishwa na zamani.
Mbali na kutungwa sera pia jamii iwe na mtazamo
chanya kuwa kazi ya sanaa ya maigizo ni kazi kama kazi nyingine, hivyo
jamii itoe ushirikiano kwa watoto wanaopata mafunzo ya sanaa na kujiunga
katika tansia hiyo.
Wataalamu wanasemaje?
Mratibu wa Mradi wa Kujenga Weledi wa Sanaa za
Maonyesho Tanzania, Eliachim Malimi anasema kukosa weledi na uhaba wa
elimu ya kutosha kwa watu wanaofanya uandishi wa sanaa za maonyesho ni
kikwazo kwa wasanii wengi kushindwa kufanya vizuri kwa tasnia hiyo.
Malimi anasema wasanii licha ya kuwa na vipaji,
lakini havisaidii kama hawajapitia mafunzo ambayo ndiyo humfanya msanii
kuwa na uwezo wa kubuni na kufanya kazi yake kwa ufanisi na hivyo kuwa
uandishi mzuri wa sanaa za maonyesho na tamthiliya.
“Weledi ubunifu na elimu ni vitu vikuu anavyotakiwa kuwa navyo
mtu kwenye uandishi wa sanaa za maonyesho na hii itamsaidia msanii aweze
kufanya vizuri katika tasnia hii,” anasema Malimi.
Malimi ambaye kwa sasa anatoa mafunzo katika
vikundi vitatu vilivyopo chini ya Kampuni ya Parapandani ambavyo ni
Sanaa ya maigizo vya Malezi Youth Theather, Lumumba na Parapanda.
Anasema Parapanda ni Kampuni ya Sanaa ya Maonyesho
inayojihusisha na sanaa na ina miaka 20 sasa tangu ilipoanzishwa, lengo
kuu la kuanzishwa ni kutoa mafunzo ya sanaa kwa watoto wadogo ili
kurudisha sanaa ya utamaduni.
Malima anasema lengo la kutoa mafunzo ya sanaa kwa
vijana ni kuleta matumaini kwa vijana wadogo katika kazi za sanaa na
uandishi wa maonyesho pamoja na tamthiliya.
Anasema mwaka 2012 kampuni hiyo ilifanya miradi
mbalimbali ya maendeleo ikiwiwemo miradi ya Shirika la Kazi Duniani
(ILO), Matokeo Makubwa Sasa (BRN) na Umoja wa Ulaya ambako walikuwa
wanafanya uhamasihaji kupitia sanaa.
“Tumeamua kutoa mafunzo kwa wasanii wetu ili
kuwajengea weledi wa kuandika kwa ufasaha tamthiliya na uandishi wa
sanaa za maonyesho, ili waweze kupata masoko na kukuza sanaa ya uandishi
wa maonyesho,” anasema Eliachim.
Anatolea mfano Kikundi cha Lumumba Theatre
kimefanya vizuri katika onyesho la maigizo ya Kinjekitile Ngwale katika
vita vya Maji Maji 1905-1907 kupitia kitabu kilichoandikwa na mwandishi
na mtunzi mahiri wa vitabu na riwaya nchini, Ibrahim Hussein 1969 na
kuchapwa tena 1981.
Malimi anasema kikundi hicho cha Lumumba Theatre
kiliamua kufanya sanaa hiyo ya maigizo ya mpiganaji huyu, ambaye
alianzisha vita vya Maji Maji wakati wa mapambano dhidi mkoloni wa
Kijerumani.
“Kujenga weledi kwa msanii ndiyo nguzo muhimu ili
weweze kuandika andishi nzuri la tamthilia litakalomwezesha kuvutia
watazamaji au wasikilizaji ili waweze kupata soko la ndani au nje ya
nchini kupitia sanaa za ngoma na maonyesho,” anasema.
“Tunatumia mbinu hizo ili kufikisha ujumbe kwa
jamii ili iweze kuelewa kwani ujumbe wa sanaa ya maonyesho ndiyo njia
rahisi kwa jamii kuweze kuelewa kuliko hata mkutano,” anasema Malimi.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo kutoka Kikundi
cha Lumumba, Ahmad Madai anasema mafunzo hayo yatamsaidia katika kazi za
sanaa ya maigizo kwa sababu hapo awali alikuwa akifanya kazi chini ya
ubora kwa kukosa mafunzo.
“Kitu kipya nilichokipata katika mafunzo haya ni
namna ya uandishi wa mchezo kwa sababu hapo awali tulikuwa tunacheza
bila taaluma, lakini kupitia mafunzo ya darasani sasa sanaa ya maigizo
tutaifanya kwa weledi na ubunifu mkubwa,” anasema Madai.
Nini kifanyike
Mandai anasema ili tasnia ya sanaa ya maigizo
isonge mbele Serikali haina budi kutoa msaada wa kutosha siyo, kusubiri
viongozi wakubwa wa dunia kuja na kuwatafuta wasanii wa ngoma za asili
na waandishi wa sanaa za maonyesho bali kujenga uwezo kwenye soko la
ndani katika majukwaa.
Kwa nini mafunzo hayo
Mwongozaji wa filamu wa sanaa kutoka Kikundi cha
Parapanda Theatre Lab Trust, Amani Lukuli anasema lengo la kutoa mafunzo
hayo ni kuvifanya vikundi viwe na utawala mzuri na kuepuka kugawanyika
pamoja na kuwa na uwezo wa kuandaa kazi zao wenyewe kupitia bajeti zao
na siyo kusubiri wahisani.
Changamoto zilizopo
Lukuli anasema moja kati ya changamoto zilizopo
katika tasnia ya sanaa ni kwamba Sanaa za maonyesho zipo chini, lakini
kupitia mafunzo hayo wanaweza kupeleka ushawishi kwa jamii hasa baada ya
kutumika katika uhamasishaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ya leo
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment