Askofu Mkuu wa Kanisa la kiinjili la kiluther Tanzania (KKKT), Dk Alex
Malasusa (kushoto) akimsimika Mchungaji Dk Fedrick Shoo kuwa Askofu mpya
wa KKKT Dayosisi ya kaskazini katika ibada iliyofanyika jana katika
usharika wa Moshi mjini.
Askofu mpya wa Dayosisi ya Kaskazini ya Kanisa la Kiinjili la
Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk Fredrick Shoo jana alitoa ujumbe mzito kwa
Rais Jakaya Kikwete alipomtaka kuwawajibisha haraka wahusika kwenye
kashfa ya escrow kwa kuwa “viporo vinaumiza tumbo”.
Dk Shoo aliyemrithi askofu Dk Martin Shao
aliyestaafu, alitoa kauli hiyo mbele ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais
(Utawala Bora), George Mkuchika ambaye alimwakilisha Rais, wakati
akihutubia kwenye ibada ya kuwekwa kwake wakfu na kusimikwa kwa msaidizi
wake, Mchungaji Elingaya Saria iliyofanyika Usharika wa Moshi Mjini.
Mbali na Waziri Mkuchika, wengine waliokuwapo
kwenye ibada hiyo ni mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na
Edward Lowassa, pamoja na Waziri wa Maliasili na Utalii, Lazaro
Nyarandu. Pia walikuwapo baadhi ya wabunge na maaskofu wa dayosisi 24.
Katika hotuba yake, Dk Shoo alisema kanisa
linasikitishwa na ufisadi mkubwa unaoendelea miongoni mwa viongozi na
watumishi wa umma na kiburi wanachokionyesha wanapoelezwa ukweli.
“Kinachotusikitisha zaidi ni wahusika kuonyesha
jeuri kubwa na ukakamavu wa hali ya juu pale wanapoambiwa,” alisema Dk
Shoo huku akishangiliwa.
“Mimi sioni mantiki kama mtu amehusika katika mambo fulani, halafu anaanza kusema sikueleweka vizuri halafu anajiuzulu.”
Ingawa hakumtaja kwa jina kiongozi huyo, Jaji
Fredrick Werema alijiuzulu nafasi yake ya Mwanasheria Mkuu kwa
kumwandikia barua Rais akieleza kuwa ushauri wake katika suala la escrow
haukueleweka na umesababisha tafrani.
Katika sakata hilo la Escrow, Jaji Werema ndiye
anayedaiwa kuandika barua akieleza kuwa fedha zilizokuwa kwenye Akaunti
ya Tegeta Escrow zilipwe IPTL bila ya kukatwa kodi.
“Tunatambua Rais ameanza kuchukua hatua dhidi ya
watu kama hawa. Tunazidi kumwombea yeye na Serikali yetu ili wamwonyeshe
hatua zaidi zinazofaa kuchukuliwa,” alisema Askofu Shoo.
“Panapohitajika kuchukua hatua, tusiweke viporo.
Unajua viporo vikishakuwa vya muda mrefu, vinaumizaa tumbo,” alisisitiza
Dk Shoo huku umati uliofurika ukilipuka kwa furaha na makofi.
Akitangaza uamuzi wake kuhusu maazimio ya Bunge la
Muungano, Rais Kikwete alitangaza kumwondoa kazini Profesa Anna
Tibaijuka, aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi,
lakini akasema amemweka kiporo Waziri wa Nishati na Madini, Profesa
Sospeter Muhongo.
Wanasiasa kujipitisha
Askofu Shoo pia hakuwasitiri wanasiasa wanaopita makanisani na misikitini kutafuta umaarufu ili uwanufaishe kupata madaraka.
“Sisi tunapenda kuwaasa wasaka madaraka kama hao,
wanaokimbilia kusaka umaarufu rahisi, tunawatambua na tutawatambua kwa
rangi zao,” alisema askofu huyo.
“Ningependa ijulikane kwa wanasiasa na waumini
wote kwamba nyumba za ibada ni mahali patakatifu. Si mahali pa kufanyia
usanii. Sina maana kila mwanasiasa ni msanii.
“Kanisani ni mahali panapotakiwa kukaribiwa kwa
hofu na kwa uchaji. Siyo uwanja wa siasa. Tumpe Mungu yaliyo ya Mungu na
ya Kaisari yaliyo ya Kaisari lakini pasipo kuharamisha unabii.”
Kuhusu Panya Road
Katika hatua nyingine, Askofu Shoo alisema kuibuka
kwa kundi la wahalifu maarufu kama Panya Road jijini Dar es Salaam ni
matokeo ya vijana wengi nchini kukosa ajira.
“Ajira kwa vijana ni changamoto kubwa kutokana na
kufungwa kwa viwanda vingi vilivyokuwapo, matokeo yake wengi wanaokaa
bila ajira, wamejiingiza katika ajira zisizofaa,” alisema.
Dk Shoo alisema kama hali ya vijana wengi kukosa
ajira itaendelea kama ilivyo sasa, itakuwa ni hatari kubwa kwa usalama
wa nchi na kuonya kuwa watu waliokata tamaa ni vigumu kuwatawala.
“Watu watakata tamaa na watu waliokata tamaa
hawatawaliki. Tukiendelea hivi tusishangae hao wanaoitwa Panya Road
wakajitokeza hata hapa Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro,” alisema.
Askofu Shoo alisema Tanzania si masikini na kwamba
nchi imejaliwa utajiri mwingi na kusisitiza kuwa wanaosema Tanzania ni
maskini na kuamini hivyo, ni maskini wa fikra
“Tunachohitaji ni viongozi na watumishi wenye roho ya uzalendo.
Bila hivyo ni vigumu kuhakikisha kuwa rasilimali za nchi hii
zinawanufaisha Watanzania wote,” alisema.
Mkuchika ajibu
Akijibu hotuba hiyo iliyoonekana kuwa mwiba mkali
kwa Serikali, Mkuchika alisema Serikali imekwishachukua hatua na
itaendelea kuchukua hatua dhidi ya watu wote waliohusika na sakata la
escrow.
“Tayari wahusika wamechukuliwa hatua. Mfano
Mwanasheria Mkuu wa Serikali amejiuzulu na Waziri mmoja ameondolewa
katika Baraza la Mawaziri,” alisema Mkuchika katika hotuba yake.
Mkuchika alisema hata Katibu Mkuu wa Wizara ya
Nishati na Madini, Eliakim Maswi amesimamishwa kazi ili kupisha
uchunguzi na kwamba uchunguzi dhidi ya watu wengine waliotajwa bado
unaendelea.
“Kwa wale wengine ambao uamuzi bado haujafikiwa,
vyombo vya dola, kama (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa)
Takukuru na Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, vinavifanyia
kazi,” alisema.
Mkuchika alimpongeza Askofu Shoo kwa kutambua
tatizo la wanasiasa kutumia makanisa na misikiti kunadi sera zao, lakini
akawashauri viongozi wa dini kutowakaribisha wanasiasa hao ili
kukomesha hali hiyo.
“Endapo viongozi wa dini watakataa, tatizo hili
halitakuwepo. Msiwakaribishe kutumia maeneo ya kanisa na misikiti
kuhubiri siasa. Tusichanganye dini na masuala ya siasa,” alisisitiza
Mkuchika.
Dk Malasusa atoa angalizo
Mkuu wa Kanisa la KKKT, Dk Alex Malasusa alisema
mwaka 2015, nchi ina mambo mengi, lakini ni vyema Serikali ikaweka
kipaumbele katika mambo muhimu zaidi, likiwamo Daftari la Wapigakura.
“Serikali iboreshe Daftari la Wapigakura ili wananchi wengi
waweze kujiandikisha na kupiga kura. Mnasema tuendeleze amani lakini
amani haiwezi kuwepo kama haki haipo,” alisema.
Askofu Malasusa pia alitahadharisha kuibuka kwa
vikundi vya uhalifu kama Panya Road na kudokeza kuwa Moshi kumeibuka
kundi la Kanyaga Twende.
Dk Malasusa alimwambia Mkuchika kuwa suala la
utawala bora si la Rais, bali ni la kwake na kumtaka asimamie utawala wa
sheria vinginevyo, mwisho wa kuibuka vikundi hivyo utakuwa mbaya.
Chanzo:Mwananchi
Chanzo:Mwananchi
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
0 comments:
Post a Comment