Home » » ASKOFU KATOLIKI:MAUAJI ALBINO YANAAIBISHA TAIFA.

ASKOFU KATOLIKI:MAUAJI ALBINO YANAAIBISHA TAIFA.

Askofu Isaac Aman wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Moshi, akimpongeza Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Dk. Reginald Mengi, muda mfupi baada ya kumaliza kuchangisha fedha katika harambee ya uchangiaji wa ujenzi wa Shule Maalum ya Sekondari ya St. Pamachius Inclusive (Pamakio) mjini Hai, itakayohudumia watoto wenye ulemavu nchini. Katika harambee hiyo Mengi alichangia Sh. bilioni moja. PICHA:GODFREY MUSHI
Askofu wa Kanisa Katoliki, Jimbo la Moshi, Isaac Aman, amesema mauaji ya kikatili dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi (Albino) yanayoendelea nchini, yataififisha Tanzania isiitwe kisiwa cha amani.
 
Askofu Aman alisema hayo mjini hapa juzi, wakati wa harambee ya kuchangisha zaidi ya Sh. milioni 800 za ujenzi wa Shule Maalum ya Sekondari ya St. Pamachius Inclusive (Pamakio), yenye upendeleo maalum kwa watoto wenye ulemavu na wenye uwezo wa kumudu masomo ya sekondari.
 
Shule hiyo ambayo ujenzi wake hadi kukamilika kwake itagharimu Sh. bilioni sita, inajengwa na Kanisa Katoliki katika kijiji cha Kimashuku, wilayani ya Hai, mkoani Kilimanjaro. 
 
Katika harambee hiyo, Mwenyekiti wa IPP, Dk. Reginald Mengi, aliahidi kuchangia Sh. bilioni moja.
 
Askofu Aman alisema kama Watanzania wangeelimishwa vizuri kuhusu hazina ya vipaji na karama walizonazo watu wenye ulemavu nchini na kuvifanyia kazi, utajiri uliopo ndani yao ni mkubwa kuliko utajiri wa gesi na mafuta. 
 
Alisema Tanzania inashangaza ulimwengu kutokana na baadhi ya watu kuwa na imani potofu kwamba, viungo vya walemavu huvuta bahati na utajiri.
 
“Wengine huona aibu ya kuchekwa na kuwaficha; baadhi yao huwaua kwa siri kwa kuogopa gharama za kuwahudumia…nawaalika tufungue utamaduni mpya wa kuwafanya huru watoto waliofungwa kwa ulemavu, wasikate tamaa, wakaishia kukaa majumbani na hata kuwa omba omba,” alisisitiza Askofu huyo.
 
Alifafanua kuwa, shule hiyo imepewa jina hilo kwa kuwa Mtakatifu Pamachius wa Dola ya Roma, alikuwa rafiki mkubwa wa watu wasioona (vipofu), masikini na walemavu wa aina mbalimbali.
 
Kwa upande wake, Dk. Mengi, alisema jamii inapaswa kubadili fikra potofu kuhusu watu wenye ulemavu na siyo kuwasaidia huku wakiwanyooshea vidole.
 
“Mimi ni bomba la kupeleka maji ya kunywa kwa watu wenye kiu. Sasa ndugu zangu ifike mahali, tujiulize ni kwa nini mimi nimezaliwa kwenye ardhi yenye rutuba, utajiri na amani, sijazaliwa mlemavu au kupata ulemavu baada ya kuzaliwa. Ulemavu ni mapenzi ya Mungu. Najua vyote nilivyo navyo ni kwa mapenzi yake; ndiyo maana tumeitwa hapa tutoe sadaka kwa ajili ya wenzetu,” alisema Dk. Mengi. 
 
Katika harambee hiyo, Dk. Mengi alichangia shilingi bilioni moja, huku akiahidi kutoa Sh. milioni 200 kila mwaka kama sehemu ya sadaka yake.
 
Mbali na mchango wake, Dk. Mengi, alichangisha fedha zaidi ya Sh. milioni 430.8 kutoka kwa wafanyabiashara wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro, waumini na wadau wa elimu nchini.
 
CHANZO: NIPASHE
Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa