Home » » TATIZO LA POMBE ROMBO LACHUKUA SURA MPYA

TATIZO LA POMBE ROMBO LACHUKUA SURA MPYA

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

 
Tatizo la unywaji pombe wa kupindukia kwa wanaume wilayani hapa, limechukua sura mpya baada ya jeshi la polisi mkoa wa Kilimanjaro kutuhumiwa kushiriki kuchochea biashara hiyo.
 
Akiongea katika mkutano wa hadhara kuhusu tatizo hilo, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alisema kuwa taarifa mbali mbali zinaonyesha kuwa baadhi ya askari si waaminifu katika vita dhidi ya pombe haramu inayoendelea hivi sasa wilayani humo.
 
“OCD taarifa zinaonyesha kuna baadhi ya askari wako, ambao wanashirikiana na wafanyabiashara wa pombe haramu ya gongo na hili linafanya kazi ya operesheni kukomesha tabia hii mbaya kuwa ngumu,” alisema. Alisema taarifa hizo zikiwamo zile za kutoka kwa wananchi wenye nia njema na vita hiyo, zinaonyesha kuwa baadhi ya askari wasio waaminifu wamewageuza wafanyabiashara wa gongo kuwa ATM zao (mashine za kutolea pesa) kwa kuchukua rushwa hivyo kusababisha uovu huo uendelee. 
 
Gama alisema serikali haijamzuia mtu kunywa pombe halali ili mradi isiwe ni wakati wa kazi na kwamba pale itakapobainika kuna wanao kunywa wakati wa saa za kazi watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria.
 
“Inasikitisha kusikia kuwa baadhi ya pombe zinazonyweka Rombo zimetengenezwa na mbolea aina ya urea, maji ya betri, spiriti, kinyesi cha binadamu, sukari guru na molasesi, hii ni hatari kwa afya ya mwanadamu,” alisema.
 
Kwa upande wake Padri Serafini Kilawe, wa Kanisa Katoliki, alisema kuwa vita dhidi ya pombe haramu hasa ya gongo haitaweza kumalizika iwapo baadhi ya askari hawataacha kushirikiana na wanaotengeneza pombe hizo.
 
Suala la ulevi uliokithiri limekuwa gumzo  maeneo mbali mbali mkoani Kilimanjaro na nje ya mkoa huo, ambapo imedaiwa kuwa baadhi ya wanawake wilayani humo wanalazimika kukodi wanaume kutoka nchi jirani ya Kenya ili kukidhi mahitaji yao ya kindoa.
 
Wananchi waishio wilayani hapo, Elizabeth Shabani na Mary Shirima, walikiri kuwapo kwa askari, wanaofika maeneo wanapotengenezea pombe haramu  kuchukua fedha kila mwisho wa mwezi kama ni ujira wa kuwalinda.
SOURCE: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa