Home » » Wakemea vitendo vya rushwa ndani ya polisi

Wakemea vitendo vya rushwa ndani ya polisi

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 

Viongozi wa dini mkoani Kilimanjaro, wameonya vitendo vya baadhi ya polisi wanaojihusisha na vitendo vya rushwa na upendeleo kuelekea uchaguzi wanaweza kusababisha machafuko.
Walitoa tahadhari hiyo juzi, mbele ya Naibu mkuu wa jeshi hilo, Abdulrahman Kaniki (pichani) na Naibu waziri wa Mambo ya Ndani, Pereira Ame Silima, wakati wa hafla ya ufungaji wa mafunzo ya awali ya askari 3,497 wa polisi na Uhamiaji, yaliyofanyika Shule Kuu ya polisi-Moshi (MPA).

Padri, Daniel Amani wa Kanisa Katoliki, jimbo la Moshi, aliwataka askari hao kuliepusha taifa kuingia katika machafuko kutokana na tamaa ya mali na fedha zisizo halali na upendeleo kwa baadhi ya wagombea wa nafasi za urais, ubunge na udiwani.

Mchungaji, Sara Urassa wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini, aliwataka polisi kulinda raia na mali zao na kujitenga na rushwa ambayo hivi sasa inaonekana kuwa sehemu ya ujira wao.

“Ridhikeni na mishahara yenu hata kama ni midogo, na wala msijilimbikizie mali na kutaka utajiri kwa kuwaumiza raia. Wakati huu wa uchaguzi jiepusheni na rushwa na upendeleo kwa chama fulani,” alisisitiza.

Naibu mkuu wa jeshi hilo nchini, Kaniki aliwaasa polisi kuitikia wito huo wa viongozi wa dini kwa kujitoa kwa dhati kulinda usalama na ustawi wa jamii kwa gharama yoyote.

Silima alisema kwa kuwa rushwa hutafsiriwa kama panya wa mfalme, askari wanapaswa kujihadhari nayo.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa