Home » » Naibu Waziri aagiza waliouza jengo la Saccos wakamatwe.

Naibu Waziri aagiza waliouza jengo la Saccos wakamatwe.

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399. 
Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha.
Naibu Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, William ole Nasha, ametoa siku 14 kwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) Mkoani Kilimanjaro kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi, kufanya uchunguzi na kuwafikisha mahakamani wahusika waliouza mali ya Ushirika ya Jengo la Saccos ya Sanya Juu.
 
Aidha amemwagiza Mrajisi wa Vyama vya Ushirika nchini,  kuwachunguza Fanuel Uroki, ambaye ni Ofisa Ushirika Wilaya ya Siha na Shosi Monyo, Kaimu Mrajisi Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, wanaotuhumiwa kuuza jengo hilo na kufilisi mali za wanachama wa chama hicho.
 
Ole Nasha alitoa amri hiyo jana wilayani Siha mkoani Kilimanjaro, alipotembelea Saccos hiyo ambayo imefilisiwa na vigogo hao kwa kushirikiana na mwenyekiti na katibu wake. 
 
Alisema kwa mujibu wa malalamiko ya baadhi ya wanachama wa Saccos hiyo, Eveline Mmasai na Joseph Mmari,  ambao walizungumza kwa uchungu, Saccos hiyo ilipoanzishwa mwaka 2006 ikiwa zaidi ya wanachama 100.
 
Wanachama hao walisema walijinyima na kuwekeza ili kunufaika ikiwamo kusomesha watoto na kukopa fedha kwa ajili ya kufanya biashara kama vile kilimo na uuzaji wa mboga.
 
Lakini katika hali isiyo ya kawaida, walisema Monyo alileta kampuni ya kifaransa iitwayo USAWA ambayo mrajisi huyo alithaminisha mali za Saccos hiyo kwa kushirikiana na Mwenyekiti, Filex Mosha na Katibu wake Sinorita Orota, bila kuwashirisha wanachama.
 
Naye mjumbe wa bodi ya muda aliyeteuliwa na wanachama kufuatilia hatima ya fedha zao baada ya wanachama kuvunja bodi ya awali inayotuhumiwa kuuza jengo la wanachama pamoja na fedha zao Sh. milioni 160, Stephen Sekemi, alisema walifuatilia  fedha zao kwa kukamata mali za mwenyekiti na katibu ili wauze na wanachama wapewe fedha zao.
 
Alisema wakati wakiendelea na hatua za kukamata mali zao,  Monyo na Uroki waliwazuia kwa madai kwamba sheria haiwapi mamlaka ya kuwakamata bali waende mahakamani na wanachama walichanga Sh. milioni moja ili wapate mwanasheria kusimamia kesi waliyoifungua.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa