Imeandikwa na Nakajumo James, Moshi
WADAU wa maendeleo wameombwa kuchangia sekta muhimu ikiwamo afya ya
wajawazito na watoto chini ya miaka mitano, kwa kuhakikisha wanapata
vifaa tiba katika kuepuka vifo visivyo vya lazima.
Mbunge wa Viti Maalumu mkoani Kilimanjaro, Shally Raymond alisema
hayo wakati anakabidhi msaada wa mashuka 60 kwa kituo cha afya kata ya
Bomambuzi Manispaa ya Moshi kwa ajili ya wadi ya wanawake wajawazito na
watoto chini ya miaka mitano.
“Msaada huu wa mashuka tumeshirikiana na viongozi wa Manispaa ya
Moshi na mkoa lengo likiwa ni kusaidia wodi ya wajawazito na
watoto...wanawake wanakabiliwa na changamoto kubwa sana, tunahitaji
kuwapatia misaada zaidi,” alisema.
Akiwa amefuatana na baadhi ya viongozi wa Umoja wa Wanawake Tanzania
(UWT) wa kata ya Bomambuzi, Mbunge huyo alisema amekusudia kushiriki
kupunguza vifo vya wajawazito na watoto.
Mbunge alikuwa akizungumzia mradi wa kuboresha afya ya uzazi kwa
kushirikiana na umoja wa vilabu vya wanahabari nchini (UTPC), Mtandao wa
Wadau wa Kuboresha Upatikanaji wa Uzazi wa Mpango (Tanzania Coalition
for Access to Contraception –TCAC) na Marie Stopes Tanzania (MST).
Kwa upande wake, Mratibu wa Afya ya Uzazi na Mtoto mkoa wa
Kilimanjaro, Fatina Rashid, alisema takwimu za mwaka 2014, zinaonesha
Wilaya ya Siha ilikuwa na vifo vitatu kati ya vizazi hai 1,000.
Halmashauri nyingine na idadi ya vifo kwenye mabano kati ya vizazi
hai 1,000 ni Hai (3), Moshi Vijijini (1) , Mwanga (4), Rombo (1), Same
(2) na Manispaa ya Moshi (14). Mwaka 2015 wilaya ya Siha ilikuwa na vifo
2, Hai vifo vitatu, Moshi Vijijini kimoja, Mwanga vifo viwili, Rombo
kifo kimoja, Same kimoja na Manispaa ya Moshi ilikuwa na vifo 23.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment