SERIKALI mkoani Kilimanjaro imetaka Hifadhi ya Taifa ya Mlima
Kilimanjaro (Kinapa) kwa kushirikiana na Ofisi ya Maji ya Bonde la
Pangani (PBWO), kuandaa taarifa za kitaalamu zinazoonesha jinsi mlima
huo ulivyopunguza maji yake kwenda katika mabwawa ya kuzalisha umeme.
Mlima Kilimanjaro umetajwa kama chanzo kikuu cha maji katika bwawa la
Nyumba ya Mungu na Hale mkoani Tanga ambayo kwa pamoja hutumika kwa
ajili ya kuzalisha umeme.
Katika taarifa iliyotolewa na Ofisa Habari wa Mkoa wa Kilimanjaro,
Shaban Pazi, inaeleza Mkuu wa Mkoa huo, Said Meck Sadiki alisema hayo
baada ya kupokea taarifa ya Mhifadhi Mkuu wa Kinapa, Beitrita Loibooki
aliyekuwa akielezea taarifa ya maendeleo ya hifadhi hiyo na changamoto
zake.
“Pamoja na taarifa yako inayoonesha kwamba mlima huu unachangia zaidi
ya asilimia 80 ya maji katika mabwawa hayo... bado hili ni jambo la
kulitazama kwa jicho la pili, nipeni taarifa ya kitaalamu inayoonesha
maji yatokayo mlima Kilimanjaro kwenda katika mabwawa hayo yamepungua
kwa kiasi gani,” alisema.
Alisema kutolewa kwa taarifa hiyo kutatoa picha halisi ya jinsi
athari za uharibifu wa mazingira na mabadiliko ya tabianchi kunavyoweza
kuathiri mazingira na namna gani inaweza kuathiri shughuli za kiuchumi.
Alisema taarifa hiyo pia itaonesha jinsi kupungua kwa maji katika
mlima Kilimanjaro unavyoweza kuathiri vyanzo vya maji na mito, jambo
litakalosababisha upungufu wa maji majumbani na viwandani na kuathiri
maisha ya kila siku.
Kwa upande wake, Mhifadhi wa Kinapa, Loibooki alisema mlima huo
unachangia maji katika mabwawa hayo ya kuzalisa umeme kwa asilimia 80 na
kwamba kama mazingira ya mlima huo hayatatunzwa ipasavyo upo uwezekano
wa mabwawa hayo yakashindwa kuzalisha umeme kama ilivyotakiwa.
CHANZO: HABARI LEO
0 comments:
Post a Comment