ZAIDI ya wanaume 200 wamezikimbia familia zao na kuziacha katika hali
duni na kwenda kusikojulikana kwa kisingizio cha kukosa shughuli za
kiuchumi baada ya kufungwa kwa Bwawa la Nyumba ya Mungu wilayani Moshi.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wanawake wamedai watoto wao wapo
hatarini kukatisha masomo kutokana na kukosa chakula, mahitaji ya shule
zikiwemo sare.
Wakizungumza na Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba katika mkutano
wa hadhara uliofanyika katika Kijiji cha Mikocheni, Kata ya Arusha
Chini, wanawake hao Asha Ndive na Sakina Abdallah walidai maisha
yamekuwa magumu.
"Tangu serikali imelifunga bwawa hili Julai mosi, hali ya kiuchumi
imekuwa mbaya na wanaume wametukimbia, tumebaki wenyewe na watoto...
mkuu wa wilaya tusaidie chakula ili angalau tumudu haya maisha wakati
tukitafuta shughuli nyingine,” alisema Asha.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kijiji hicho, Koromo Kweinasi pamoja
na kukiri kukimbia kwa wanaume hao, ameomba serikali kuainisha mipaka ya
bwawa hilo ili wananchi wafahamu eneo halisi kwa ajili ya shughuli za
kibinadamu.
“Serikali imefunga bwawa, imekataza ufugaji na kilimo pembezoni mwa
bwawa, lakini wakati mwingine tunafanya haya bila kujua, tunaomba mipaka
ya bwawa iainishwa ili nasi tuiheshimu vinginevyo tutaadhibiwa kila
siku,” alisema Kweinasi.
Alisema kijiji hicho chenye kaya zaidi ya 3,894 zinahitaji msaada wa
chakula kwani hapo awali walikuwa wakitegemea shughuli za uvuvi pekee na
sasa serikal imezisitisha.
Akijibu kauli za wananchi hao, Kippi alitaka mtendaji wa kata kuandaa
takwimu za idadi ya kaya zinazohitaji msaada wa chakula na makisio ya
mahitaji halisi ili serikali itoe.
Alisema msimamo wa serikali juu ya kusitisha uvuvi upo pale pale
lakini akataka wananchi kuuheshimu ili ijaribu kulegeza masharti
kulingana na mazingira yatakavyorejea katika hali yake.
Chanzo Na Habari Leo
0 comments:
Post a Comment