Mwonekano wa baadhi ya nyumba katika moja ya vijiji kata ya Usangi,nyumba hizo zimejengwa milimani lakini miundombinu ya umeme imewafikia
Huu ni mradi wa maji uliopo katika kijiji cha Kirogwe kata ya Usangi,hiki ni kipimo kinacho onesha maendeleo katika kijiji Hicho
Huu ni mradi wa maji uliopo katika kijiji cha Kirogwe kata ya Usangi,hiki ni kipimo kinacho onesha maendeleo katika kijiji Hicho
Imeandaliwa na Abeid Othman
Hivi karibuni,
nilifanya ziara ya siku kadhaa katika kata ya Usangi iliyopo Wilaya ya
Mwanga mkoani Kilimanjaro.
Ni ziara iliyoratibiwa na asasi ya Twaweza kwa
minajili ya kupata picha halisi ya maisha ya Watanzania wa kada za chini.
Kupitia ziara hiyo,
nilipata fursa ya kuwa karibu na
Watanzania wa vijijini, huku nikijifunza kwao kuhusu Wanachofikiri na wanachotamani kwa ustawi wa maisha yao na maendeleo ya nchi
kwa jumla.
Ukiondoa kujichanganya kwangu na wananchi hao, ziara
ya Usangi ilinifunza mengi ambayo kwa kuandika makala haya, pengine Watanzania
wenzangu tunaweza kujifunza kutoka huko.
Kimsingi, vijiji vya Usangi na pengine mkoa mzima wa
Kilimanjaro vina tofauti kubwa ya kimaendeleo, ukilinganisha na vijiji vingi
katika maeneo mbalimbali ya nchi yetu. Usangi na mkoa mzima kwa jumla, kuna
watu wanaokumbuka kuendeleza kwao.
Wenyeji wa Usangi
wanatambua asili yao; wanajua
walikotoka ndio maana wengi huamua
kurudi kwao kila mwisho wa mwaka. Ni dhahiri kuwa wanarudi katika maeneo
waliyoyaendeleza; wanajua pa kufikia kama familia.
Nilichokiona huko
ni kuwapo kwa nyumba nyingi za kifamilia tena zikiwa sehemu moja. Huu ni
utamaduni unaopaswa kuigwa na watu wengine.
Nilikuwa nasikia taarifa za umeme kufika mpaka
kwenye mashamba ya migomba, hili nimeliona kwa macho yangu.
Kama
haitoshi, kuna miundombinu ya maji ya bomba hadi maeneo ya milimani. Yote haya
ni kwa sababu ya kuwapo kwa wawakilishi wa wananchi wanaojitambua na mwamko wa
wakazi wake.
Wasomi wao nao walisoma na kuamua kurudi nyumbani
kuendeleza; hawakusoma ili wajitenge na watu washamba vijijini mwao.
Ukifika Usangi
kwa mfano, ni rahisi kujuzwa kuwa hapa ni kwa mzee David Msuya (Waziri
Mkuu Mstaafu, pale kwa kina Asha-
Rose Migiro (Waziri katika serikali ya
awamu ya nne) na viongozi wengine wengi wastaafu na walio madarakani.
Kwa sababu ya
umakini wa wakazi, kijiji kama Kirongwe nilichoishi kwa siku kama tatu hivi na vingine vya jirani vimeendelea kiasi
cha kuvifananisha na mji mdogo.
Katika vijiji hivi
nimeshuhudia ujenzi wa nyumba za kisasa yakiwamo maghorofa, usafiri wa
kuaminika. Haya ni muhali kuyakuta katika vijiji vingi nchini. Miaka ya nyuma, nilifanya
ziara katika kijiji cha Lula Kawala
mkoani Rukwa.
Nilikuta shule ya kijiji ikiwa haina madawati, huku wanafunzi wakirundikwa darasani kama matenga ya viazi.Cha ajabu, mita chache kutoka shuleni kulikuwa na shamba kubwa la miti ya mbao.
Halikuwa shamba la mwekezaji kutoka nje, bali la
watu ambao ni wazaliwa wa eneo hilo, lakini hawakuona haja ya kutumia rasilimali
hiyo kwa ajili ya kuwanusuru watoto wao. Naamini hili haliwezi kutokea mkoani Kilimanjaro.
Najua wapo wanaoweza kunikosoa kwa kudai Usangi na
hata wilaya nzima ya Mwanga, imeendelea kwa sababu ya kuwapo kwa viongozi
waliojipendelea kupeleka maendeleo huko walipokuwa madarakani.
Pengine kuna ukweli, lakini nchi hii imekuwa ikitoa
viongozi karibu kila kona, mbona haya ya Usangi hatuyaoni mahala pengine, au
kutoendeleza kwako ndio uzalendo?
Tofauti na viongozi wa Kilimanjaro wanaorudi kwao kuendeleza,
uko ushahidi wa viongozi mbalimbali wanaokimbia maeneo yao ya asili.
Wanaona aibu kurudi makwao, ndio maana wengi
wamejenga makazi ya kifahari nje ya maeneo yao ya asili. Hili halipo Moshi, ndio maana mtu anaweza
kujenga ghorofa lenye hadhi kijijini.
Nasi wengine
tuige, tuishi mijini lakini tukumbuke kuendeleza tulipotoka.
0 comments:
Post a Comment