Shughuli ya kubeba kuni kutoka chini kwenda mlimani ilipo nyumba ikiendelea
Abeid Poyo
Kutembea sana ni kujua mengi.
Na kwa hakika kama wahenga walivyosema: ‘mtembea bure sio sawa na mkaa bure.’
Ukweli ni kuwa unaweza
kutembea ukaokota kitu kikakufaa maishani.
Hiki ndicho kilichonitokea mimi,
shukrani kwa asasi makini ya Twaweza ambayo mwezi Mei mwaka huu, iliniwezesha
kwa mara ya kwanza kukanyanga ardhi ya wilaya ya Mwanga iliyopo mkoani
Kilimanjaro.
Ni ziara ya siku kadhaa
iliyonichukua katika vijiji kadhaa hasa kijiji cha Kirongwe kilichopo kata ya
Usangi.
Nikiwa Usangi ndipo nilipoona
mengi yaliyonivutia ambayo Watanzania wanapaswa kujifunza kutoka huko.
Mambo kadhaa yalinivutia
ikiwamo ujenzi wa nyumba za milimani. Ikumbukwe huku kuna maeneo makuu mawili
viko vijiji vya chini (low land) kama na
vile vya juu (high land) kama .
Wakati makazi kwa wale
wanaoshi chini ya milima ujenzi wake ni rahisi, wapo wanaojenga milimani.
Siyo kazi rahisi lakini
simulizi za wenyeji zinasema wapo watu maalumu wenye utaalamu wa kuchonga
miamba na hatimaye kupata kiwanja mlimani.
Huko nyumba itajengwa, kama
umeme utafika, maji pia na kama ni bustani au hata shamba utaliona.
Nikiwa katika kijiji cha
Kirongwe, mwenyeji wangu ambaye pia ni Mwenyekiti wa kijiji, Mzee Nasibu
Ramadhani, amejenga nyumba yake mlimani, kibarua kikawa kwangu mimi na
mwenzangu Richard Temu kupanda na kushuka kila siku, haikuwa kazi rahisi lakini
tukazoea na wakati mwingine tulilazimika kupandisha kuni kutoka chini ya mlima
kupeleka mlimani ilipo nyumba kwa ajili ya matumizi ya familia. (Angalia picha
mwenzangu, Richard akiwa na kuni akipandisha mlimani).
Wilaya ya Mwanga hasa vijiji
nilivyobahatika kutembelea vinavutia kwa ukijani wake, na haya yote tisa,
umeshaona umeme ukipita hadi kwenye mashamba ya migomba? Huku maendeleo yalishafika
siku nyingi, ndio maana sio ajabu kuona hata migombani kuna nguzo za umeme.
Hii ni wilaya ambayo wakazi
wake wa asili ni Wapare. Naam nilichovutika huko ni ukarimu wa wenyeji. Mpare
humwambii kitu kwa chai. Katika nyumba nyingi tulizotembelea aghalabu
makaribisho yaliambatana na kupewa chai. Pata picha unatembelea nyumba nne au
tano ndani ya saa mbili na kila nyumba lazima unywe chai! Ukarimu huu ni wa
aina yake.
Nilielezwa kuwa chai ni
sehemu ya maisha ya Wapare, huo ni utamaduni wao.
‘’Yaani ndio desturi yetu,
tena siku hizi watu hawana ng’ombe, ungepewa chai ya maziwa tu kila nyumba au
chakula hadi jasho likutoke, anasema mwenyeji mmoja wa Usangi aitwaye Asiatu
Msuya.
Pamoja na yote haya
niliyojionea upareni, kitu kimoja kilinishangaza. Awali nilikuwa nikijua kuwa
makande ndicho chakula mojawapo kikuu cha huko. Ajabu ni kuwa katika siku zote
nilizokaa Usangi hasa kijiji cha Kirongwe, sikuona makande mezani.
Nilipomuuliza mwenyeji
mwingine wa hukao aitwaye Ziada Kejo, alinijibu: ‘’ hapana, ni mara chache
(kula makande). Chakula kikuu ni ndizi au kishumba.
Kishumba kwa mujibu wa Ziada
ni mchanganyiko wa maharage na ndizi. Hiki ni moja ya vyakula vya Upareni kama
ilivyo kwa kirembwe. Hata hivyo siku
zangu chache za kukaa Usangi, sikubahatika kula kishumba, pengine safari ijayo
panapo majaliwa, nitaomba wenyeji wangu wanipikie kishumba.
Abeid Poyo ni mwandishi wa
masuala ya kijamii na maendeleo. 0754990083
0 comments:
Post a Comment