Niabu
Waziri wa Malisili na Utalii,Mhandisi Ramo Makani akizungumza na
wananchi katika kijiji cha Mshiri wilayani Moshi ,alipotembelea kijiji
hicho kusikiliza Changamoto zinazo wakabili hususani katika eneo la Nusu
Maili lililopo chini ya Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro.
NA HAMZA TEMBA -WMU
...............................................................................
Naibu
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhandisi Ramo makani amesema jukumu la
uhifadhi wa Maliasili za taifa sio la Serikali pekee kwakua Maliasili
hizo ni urithi wa taifa na kila mwananchi anapaswa kujua kuwa ana
jukumu la kulinda urithi huo kutokana na umuhimu wake kwa taifa na jamii
kwa ujumla.
Makani
amesema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mshiri,
Jimbo la Vunjo Wilaya ya Moshi mkoani Kilimanjaro katika ziara yake ya
siku mbili mkoani humo kwa ajili kuona changamoto za uhifadhi na kutatua
migogoro ya ardhi kwenye maeneo yaliyohifadhiwa.
Alisema
askari pekee na mitutu ya bunduki haitoshi kulinda maliasili hizo
kutokana na ukubwa wa maeneo yaliyopo ukilinganisha na rasilimali
zilizopo. "Maliasili hizi zipo kwa faida ya kila mwananchi, tunawaomba
muendelee kuiunga mkono Serikali katika kulinda Maliasili tulizonazo,
tunahitaji kufanya uhifadhi shirikishi, utalii uimarike na nchi yetu
ipate mapato zaidi tuweze kufikia uchumi wa kati", alisema Makani.
Akitaja
miongoni mwa faida hizo, Makani alisema maliasili za misitu husaidia
upatikanaji wa mvua, kuweka mazingira bora kwa ajili ya kilimo na
upatikanaji wa hewa safi. Kwa upande wa faida za kiuchumi alisema sekta
hiyo kupitia utalii inachangia asilimia 17.2 ya pato la taifa na asilimi
25 ya mapato yote ya fedha za kigeni.
Kwa
upande wake Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro,
Betrita Loibooki alisema hifadhi hiyo imejenga mahusiano mazuri na
wananchi wa vijiji jirani na kwa kiasi kikubwa imefanikiwa kukabiliana
na ujangili ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita hakuna
tukio lolote la ujangili wa tembo lililoripotiwa katika hifadhi hiyo.
Betrita
alisema katika kutekeleza agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la
uwekaji wa vigingi vya mipaka kwenye maeneo ya hifadhi ili kuepuka
migogoro na wananchi alisema jumla vigingi 290 vimewekwa kwa ushirikiano
na wananchi kuzunguka hifadhi hiyo kwa urefu kwa kilomita 123 sawa na
asilimia 100 ya lengo lililokusudiwa.
Kwa
upande wa Wananchi wa kijiji hicho cha Mshiri ambacho kinapakana na
Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro waliiomba Serikali iwalegezee masharti
waweze kuingia na waume zao pamoja na vijana wao wa kiume katika eneo la
Nusu Maili lililopo ndani ya hifadhi hiyo waweze kusaidiana kazi ya
kukata majani ya mifugo na kuokota kuni.
Akitoa
ombi hilo mbele ya Mhandisi Makani, mkazi wa kijiji hicho, Theresia
Mtui alisema wanawake wa vijiji jirani na hifadhi hiyo wanaruhusiwa
kuingia ndani ya eneo hilo kwa ajili ya kukata majani ya mifugo na
kuokota kuni kavu lakini wanaume hawaruhusiwi.
Alisema
wapo tayari kuhifadhi na kulinda mlima huo “Tunaomba mturuhusu na mtupe
angalao miaka miwili au mitatu ya majaribio muone tutakavyolinda msitu
huu”, alisema Mtui.
Mkazi
mwingine wa kijiji hicho, Estomi Benjamin Moshi alisema “Ombi letu
turuhusiwe kuingia na kukata majani tu katika eneo hili, tupo tayari
kuilinda hifadhi hii kwa taratibu tutakazopewa”.
Akijibu
ombi hilo Naibu Waziri Makani alisema, ombi hilo litaenda kufanyiwa
kazi kwa ushirikiano kati Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Wakuu wa Wilaya
zinazozunguka eneo hilo la hifadhi ambazo ni Moshi, Rombo, Hai na Siha,
Wizara ya Maliasili na Utalii na TANAPA ambapo wananchi watapewa
mrejesho wa ombi lao hilo.
Sheria
za uhifadhi zinakataza mtu yeyote kuingia na kulisha mifugo kwenye
maeneo yaliyohifadhiwa kisheria ikiwa ni pamoja na shughuli nyingine za
kibinadamu, kutokana na umuhimu wa eneo hilo kwa wananchi wanaolizunguka
na katika jitihada za Serikali kujenga uhifadhi shirikishi, Mwaka 2014
Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Kilimanjaro iliruhusu wanawake pekee
kuingia ndani ya eneo hilo umbali wa mita 800 kutoka kwenye mpaka wa
hifadhi hiyo kwa ajili ya kukata majani ya mifugo na kuokota kuni,
wanaume walizuiliwa kutokana na kujihusisha na uharibifu wa eneo hilo.
Nae
mbunge wa Jimbo la Vunjo, James Mbatia alisema ili uhifadhi uimarike ni
lazima uwepo ushirikiano wenye tija kwa Serikali, Wananchi na Hifadhi
huku akitoa rai ushirikiano huo uimarishwe kwa maslahi ya pande zote.
0 comments:
Post a Comment