Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +255765056399.
Na: Agness Moshi – MAELEZO.
Ulaji
wa nyama una faida lukuki kwa afya ya binadamu ikiwa ni pamoja na
upatikanaji wa virutubisho vya aina ya protini ambayo ni rahisi kutumika
mwilini, madini mbalimbali (Calcium, Magnesium, Phosphorus, Zinc na
Chuma); vitamini aina ya folic asidi, E, B na B12 ambayo inapatikana
katika nyama pekee.
Nyama pia inasaidia katika ukuaji na kuongeza
afya ya mlaji kutokana na uwezo mkubwa wa kujenga mwili, kukarabati
seli za mwili zilizokufa, kuzalisha chembe hai mpya, kurekebisha kinga
ya mwili, kuongeza damu na kuimarisha mifupa.
Hata hivyo faida
zote hizo zinapatikana tu, kwa walaji wa nyama iliyo bora na yenye
kiwango. Hivyo ni vizuri wananchi wakazingatia kanuni za ulaji wa nyama
yenye kiwango ili kujiepusha na athari zinazoletwa na nyama isiyo na
kiwango.
Msajili wa Bodi ya Nyama Tanzania (TMB) Bi.Suzana Kiango
amesema kuwa nyama yenye kiwango na bora huanzia kwenye utunzwaji wa
mifugo wenye kuzingatia kanuni za uzalishaji bora, unenepeshaji wa
mifugo yenye umri mdogo kwa kuwalisha chakula mchanganyiko kwa muda
usiopungua siku 90 kabla ya kuchinja.
Bi.Kiango amesema kuwa
hatua nyingine ni katika uchinjaji ambapo inashauriwa ufanyike kwenye
machinjio bora ambayo yanakidhi viwango vya usafi. Hii ni pamoja na kuwa
na sakafu na kuta zinazosafishika, maji ya kutosha na sehemu za
kuning’iniza wakati wa kuchuna na kupasua.
“Kanuni za uchinjaji
ni pamoja na kupumzisha mifugo ili kuipoteza fahamu na kumfanya mnyama
asiogope na kuzalisha asidi nyingi inayosababisha nyama kuwa ngumu, pia
iwe rahisi kutoa damu yote katika misuli. Uning’inizwaji wa chune mara
baada ya kuchinjwa unasaidia kuondoa damu iliyo mwilini. Endapo damu
haitatoka yote kwenye chune itasababisha nyama kuwa na rangi nyeusi na
kuharibika mapema”, alisema Bi.Kiango.
Madhara ya
ulaji wa nyama isiyo na viwango na bora ni pamoja na kupata magonjwa ya
tumbo, kuharisha na kutapika endapo nyama itapata vimelea vya magonjwa
hayo, kuugua magonjwa ya kuvimba miguu, kifua kikuu, shinikizo la damu,
kisukari na kansa.
Hata hivyo, Bi. Kiango amesisitiza kuwa
magonjwa haya yanaweza kuwatokea pia watu ambao hawatumii kabisa nyama
kwa hivyo si nyama pekee ndio chanzo cha magonjwa haya japo inaweza kuwa
sababu ya mtu kuugua.
“Bodi imeendelea kutoa elimu kwa
watumiaji na wachinjaji wa nyama kupitia vyombo mbalimbali vya habari
kama vile, redio, televisheni na magazeti. Pia katika maonesho
mbalimbali kama Saba saba na Nane nane ambapo wataalamu wa bodi hutoa
elimu kwa wananchi wanaotembelea mabanda ikiwa ni pamoja na kusambaza
vipeperushi” amesema Bi.Kiango.
Namna nyingine ya kutoa elimu ni
pamoja na kutumia matamasha ya nyama choma, wiki ya mayai na maonesho ya
kuku, wiki ya chakula salama na siku ya chakula duniani. Wakati wa
shughuli hizi wanashiriki hupatiwa elimu kuhusu faida na athari za kula
nyama isiyo na viwango ili kunusuru afya zao.
Aidha walaji
huelekezwa maeneo mbalimbali wanayoweza kupata nyama hiyo, na kwa
upande wa wafanyabiashara wa nyama hupewa maelekezo ya kuboresha
miundombinu ya kuzalisha, kuchinja na kuuza kwa kuzingatia viwango vya
ubora na usalama.
Kutokana na baadhi ya wafanyabiashara ya nyama
kuendelea kuwauzia walaji nyama isiyo na viwango kwa kujua au kutojua
madhara ya nyama hizo, Bi.Kiango alisema kuwa Bodi inachukua hatua za
kuhakikisha wafanyabiashara hao wanapata uelewa wa kutosha.
“Bodi
imeanza kutoa mafunzo kwa watumishi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa
ambao watashiriki katika kutekeleza majukumu ya Bodi ikiwa ni pamoja na
kusimamia uzalishaji wa nyama na kuelimisha wachinjaji ,walaji na
wadau wengine wanaojishughulisha na uzalishaji wa nyama”alifafanua
Bi.Kiango.
Aliendelea kusema mafunzo hayo yameshatolewa kwa
vitendo kwa watumishi wanne kutoka katika kila Mamlaka za Serikali za
Mitaa za mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Morogoro na Dodoma ambapo hadi
sasa jumla ya wadau 490 katika maeneo tajwa wamekwisha patiwa elimu
hiyo. Pia mafunzo yanatolewa na wadau wengine ambao ni Chuo cha nyama
cha VETA, Dodoma na Kampuni ya nyama ya jijini Arusha.
0 comments:
Post a Comment