Home » » MABALOZI 9 KUPANDA MLIMA K’NJARO KUTANGAZA UTALII

MABALOZI 9 KUPANDA MLIMA K’NJARO KUTANGAZA UTALII

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu blogzamikoa@live.com au Whatsapp namba +25576505639
Imeandikwa na Mwandishi Wetu, Moshi
Ofisa Habari Mkuu wa TTB, Geoffrey Tengeneza
KATIKA kuendeleza juhudi za kutangaza vivutio vya utalii nchini, mabalozi tisa kati yao wanane Watanzania na mmoja Balozi wa Algeria nchini Qatar, wanapanda mlima Kilimanjaro leo, ikiwa ni sehemu ya jitihada za Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) katika kuvitangaza vivutio vya nchi yetu, ukiwemo Mlima Kilimanjaro.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Moshi, Ofisa Habari Mkuu wa TTB, Geoffrey Tengeneza alisema wameandaa ziara hiyo ya mabalozi kwa lengo la kuwajengea uwezo na wigo mpana wa kuvitangaza vivutio vya utalii katika nchi watakazokwenda kuhudumia kama mabalozi. “Maandalizi yamekamilika na tunatarajia mabalozi na wafanyakazi wa Bodi ya Utalii na mjumbe kutoka Wizara ya Mambo ya Nje na waandishi wa kutoka Clouds Media Group watapanda mlima Kilimanjaro kesho (leo),” alisema Tengeneza.
Mabalozi hao wanaopanda Mlima Kilimanjaro leo ni Balozi Aziz Mlima, Balozi Samwel Shelukindo, Balozi Luteni Jenerali Wynjones Kisamba, Balozi Pastor Ngaiza, Balozi Bernard Achiula, Balozi Alan Mzengi na Balozi Antony Cheche. Pia yumo Balozi wa Algeria nchini Qatar, Abdelaziz Sebaa.
Tengeneza alisema katika kupanda mlima huo mrefu kuliko wote barani Afrika, kuna vivutio vingi watakutana navyo hivyo kuwafanya kuwa na vitu vingi vya kusimulia kama vielelezo watakapokuwa katika maeneo yao ya kazi na kuwa mabalozi wa kutangaza vivutio vya utalii ukiwemo Mlima Kilimanjaro kwa vitendo.
“Ni matumaini yetu kuwa watakwenda kuitangaza Tanzania pamoja na vivutio vyake katika nchi za nje na kufanya ongezeko la watalii kuja nchini kuongeza maradufu,” alifafanua Tengeneza. Alisema kupitia ziara hiyo, mabalozi watakwenda kutekeleza kwa vitendo Diplomasia ya Uchumi kwa kuvitangaza vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania na ukarimu wa Watanzania kwa wageni.
“Kama Bodi ya Utalii tunatoa wito kwa mabalozi wengine wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi nyingine duniani kutumia nafasi hiyo katika kuvitangaza vivutio hasa Mlima Kilimanjaro ambao ndio mlima mrefu barani Afrika,” alieleza ofisa huyo wa TTB.
Kwa upande wake, Balozi wa Algeria nchini Qatar, Abdelaziz Sebaa ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mabalozi nchini humo, alisema hiyo ni nafasi ya pekee kwake kupanda Mlima Kilimanjaro na kujionea vivutio vingine vya utalii Tanzania.
Alisema kwa nafasi hiyo na vitu atakavyokwenda kuviona, atakwenda kuwahamasisha mabalozi wengine katika umoja wao ili kuvitangaza vivutio vilivyopo Tanzania, hivyo kusaidia kujenga uhusiano mzuri zaidi katika sekta ya utalii. Ziara hiyo ya mabalozi kupanda Mlima Kilimanjaro, imeratibiwa na TTB na katika kupanda mlima huo, wataongozwa na Kampuni ya ZARA Tours iliyopo mjini Moshi.
CHANZO HABARI LEO

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa