Daniel Mjema, Moshi
TUME iliyoundwa kuchunguza vitendo vya utoaji vibali bandia kwa wageni kunakofanywa na baadhi ya maofisa uhamiaji mkoani Kilimanjaro, imekabidhi ripoti yake kwa Serikali.
Kwa mujibu wa vyanzo huru, kati ya mwaka 2009 hadi Januari 2012, Serikali ilipoteza zaidi ya Sh900 milioni kutokana na mapato ya vibali hivyo kuingia mifukoni mwa wajanja.
Habari za uhakika zilizopatikana jana zilisema kuwa ripoti hiyo ilikabidhiwa kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Mbarak Abdulwakil ambaye naye atamkabidhi waziri mwenye dhamana (Dk Emmanuel Nchimbi).
Tume hiyo chini ya mwenyekiti wake, Agustino Shio, ilifanya kazi yake kwa wiki moja ikiwahoji maofisa uhamiaji wanaotajwa kuhusika na kashfa hiyo na watoa habari huru.
Mwenyekiti huyo (Shio), alilithibitishia gazeti hili kukamilika kwa ripoti hiyo akisema kwa utaratibu uliopo, tume yake inatakiwa kukabidhi ripoti hiyo Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani.
“Sisi tumemaliza kazi yetu na kwa utaratibu tulitakiwa kumkabidhi ripoti hiyo Katibu Mkuu, Wizara ya Mambo ya Ndani na hilo tumeshalifanya,”alisema Shio.
Wakati ripoti hiyo ikikabidhiwa, mtu anayedaiwa kuwa kinara wa utoaji wa vibali bandia katika Ofisi ya Uhamiaji Moshi mkoni Kilimanjaro, anadaiwa kutamba kuwa hakuna wa kumfanya chochote akidai kuwa ‘amemalizana’ na wakubwa.
Kukabidhiwa kwa ripoti hiyo kumekuja wiki moja tu baada ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi kueleza kuwa wanaotoa vibali bandia, wana ujasiri wa kishetani.
Dk Nchimbi alisema utaratibu wa kugonga mihuri kwenye vibali kumtegemea ofisa mmoja pekee wa uhamiaji ni kumjengea ofisa huyo kishawishi cha wizi wa fedha za umma.
“Kwa utaratibu huu wa mtu mmoja kugonga mihuri, anapewa Dola 200 tunamjengea kishawishi cha kuiba. Mtu akishakuwa mwizi, anapata ujasiri wa kishetani,”alisema.
Aliongeza kuwa Ofisa Uhamiaji huyo akishapata ujasiri huo, haogopi chochote tena na akishakusanya pesa kwa wiki moja ujasiri wa kishetani unaongezeka
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment