na Charles Ndagulla, Moshi
MASHUHUDA wa ajali ya gari iliyotokea Agosti 3, mwaka huu katika daraja la mto Wona, likiwa na wahamiaji haramu 50, wametoboa siri na kupinga taarifa ya jeshi la polisi.
Gari hilo aina ya Mitsubishi Canter lenye namba za usajili T958ARB liliacha njia na kupinduka na kuwajeruhi wahamiaji haramu 27 kati ya 39 waliokutwa eneo la tukio huku 15 wakidaiwa kukimbia kukwepa mkono wa dola.
Akizungumza na Tanzania Daima mwishoni mwa wiki, mmoja wa mashuhuda wa ajali hiyo, Festo Mosha amedai kuwa wakati ajali hiyo ikitokea hapakuwa na askari yeyote wa jeshi la polisi kama inavyodaiwa katika taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari mwishoni mwa wiki.
Alidai kuwa yeye (Mosha) pamoja na mkewe na wananchi wengine ndiyo waliokuwa wa kwanza kufika katika eneo la tukio baada ya kusikia kishindo kikubwa alfajiri ya Agosti 3, mwaka huu.
Shuhuda huyo amedai kuwa baada ya kulisogelea gari hilo walishangaa kuona watu wakitoka ndani na kuanza kutimua mbio na baada ya kuangalia kwa makini walibaini kuwamo wahamiaji haramu.
Akisimulia tukio hilo kwa umakini, Mosha alisema kuwa walianza kuwapa msaada baadhi ya majeruhi kwa kuwatoa ndani ya gari na kisha alifanya mawasiliano na polisi Himo bila mafanikio na kulazimika kuwasiliana na gari la doria la FFU ambalo wakati huo lilikuwa eneo la kifaru.
“Kama RPC anasema hilo gari walilikamata Mabungo nje kidogo ya manispaa ya Moshi kwa nini hawakulipekela Moshi mjini na hao askari walienda wapi baada ya ajali hiyo kama hawachezi mchezo wa kuigiza ni nini?” alihoji.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alidai katika taarifa yake kuwa gari hilo lilikamatwa eneo la Mabungo likiwa linapakia wahamiaji haramu na ndipo polisi walipolisindikiza kuelekea kituo kidogo cha polisi cha Himo.
Kamanda Boaz anadai wakati likipelekwa kituo cha polisi, ndipo lilipoacha njia na kupinduka taarifa ambayo mashuhuda hao wanadai imetungwa kuwalinda askari wanaotuhumiwa kupokea rushwa na kuliachia gari hilo kupita karibu na kituo cha polisi Himo.
Inadaiwa kuwa gari hilo lilikuwa likitokea Taveta kwenda mikoa ya Kusini kuelekea Afrika Kusini, lakini baada ya kufika njia panda ya Himo, mawasiliano baina ya wakala wao hapa nchini ya yule wa Taveta nchini Kenya, yalipotea na kuamua kurejea Taveta ili kusubiri mawasiliano zaidi.
Gari hilo linadaiwa kupita mbele ya kituo kikuu cha polisi Himo chenye ulinzi mkali wa polisi wakiwamo wa kikosi cha farasi ambacho kipo mita kumi karibu na barabara kuu itokayo Holili kuelekea Moshi mjini.
Magari aina ya Fuso na Toyota Noah ambayo mengi yanamilikiwa na askari wa jeshi la polisi katika miji ya Tarakea, Himo, Holili na Moshi mjini, ndiyo yanayotajwa kuwa vinara wa kusafirisha wahamiaji haramu kwa ujira mkubwa.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment