Home » » KIKONGWE AUAWA KIKATILI KWA KUDHANIWA MCHAWI

KIKONGWE AUAWA KIKATILI KWA KUDHANIWA MCHAWI

Na Upendo Mosha, Same

WATU wawili wamefariki dunia mkoani Kilimanjaro katika matukio mawili tofauti, likiwamo la kikongwe, Yohana Muhamba (75), kuuwa kikatili kutokana na imani za kishirikina.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alisema Agosti 22, mwaka huu, saa mbili usiku katika Kijiji cha Njoro, wilayani Same, kikongwe huyo aliuawa akihisiwa ni mchawi.

Alisema kikongwe huyo aliuawa kwa kushambuliwa na mawe pamoja na marungu na jirani yake, Paul Mdee (49), akimlaumu kuwa ni mchawi na anamloga awe kichaa.

Alisema wanamshikilia mtuhumiwa huyo kwa kosa la kuuwa kwa makusudi na uchunguzi bado unaendelea kubaini ukweli juu ya kosa hilo.

“Jana saa mbili usiku katika Kijiji cha Njoro, Wilaya ya Same kuna kikongwe aliuawa na jirani yake kwa tuhuma kuwa ni mchawi na anamloga awe kichaa, sasa tunamshikilia mtuhumiwa kwa ajili ya mahojiano zaidi,” alisema Boaz.

Akizungumzia tukio jingine, alisema Agosti 22, mwaka huu katika Kijiji cha Kambi ya Simba, wilayani Mwanga, Michael Ambeto (27) alijiua kwa sumu ambayo bado haijajulikana.

Alisema mtu huyo alijiua kwa madai ambayo bado hayajathibitishwa na alimuua mkewe na kukimbilia katika eneo hilo kwa ajili ya kujificha na kabla ya kujiua alisikika akitaja jina la mkewe pamoja na wakwe zake, huku akionekana akili zake hazipo sawa.

Aidha, alisema wanaendelea na uchunguzi kubaini ukweli juu ya mauaji ya mwanamke huyo pamoja na mumewe kama yana ukweli wowote na yanahusika na kujiua kwa mtu huyo.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa