Home » » 'MAKARANI WA SENSA TUMIENI LUGHA NZURI'

'MAKARANI WA SENSA TUMIENI LUGHA NZURI'

Mwandishi wetu, Kilimanjaro Yetu

SERIKALI wilayani Siha Mkoani Kilimanjaro imewataka makarani wa sensa wilayani humo kuwa na kauli nzuri kwa wananchi na kuepuka kuwatoa lugha chafu zitakazowafanya wananchi wakatae kuhesabiwa.

Mbali na kuwataka kuwa na lugha nzuri pia amewataka kuvaa mavazi yenye heshima kulingana na mazingira halisi na kuepuka kunywa pombe kipindi chote cha zoezi la uhesabuji watu kwani ulevi unaweza kusababisha
karani akashindwa kufanya kazi yake kwa ufanisi.

Mkuu wa wilaya hiyo Charles Mlingwa alitoa wito huo jana wakati akifungua mafunzo ya sensa kwa makarani 133 wa wilaya hiyo ambapo alisema muonekano wa karani unaweza kumfanya mwananchi akakataa
kuhesabiwa.

“mtakapofika nyumbani kwa mtu angalieni lugha mnayotumia kila mtu anamwonekano wake wewe utakapofika na kumkuta mtu siku hiyo anahasira
angalia maneno mazuri yakuongea nae ili awe tayari kukupa taarifa sahihi na sio kuanza kumropokea na matokeo yake atakataa kuhesabiwa na hivyo kuharibu zoezi nzima”alisistiza Mlingwa.


Aidha aliwaomba viongozi wa dini, vyama vya siasa na viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya kijiji kutoa ushirikiano kwa wasimamizi wa sensa ili wananchi waweze kutoa taarifa sahihi pindi wahesabiwapo.

“Nawaamini sana viongozi wa dini na viongozi wa dini watakapo wahamasisha wananchi kutoa taarifa sahihi na kukubali kuhesabiwa naimani watatoa ushirikiano mkubwa kwenu na zoezi hili litakuwa rahisi
sana”alisema Mkuu wa wilaya.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo ofisa upelelezi wa wilaya hiyo Lutisia Mwakyusa aliwataka waliopata nafasi ya kushiriki mafunzo hayo kuzingatia kanuni na taratibu za zoezi hilo na kamwe wasiweke mbele maslahi yao na badala yake watangulize uzalendo wanchi kwani zoezi hilo ni muhimu kwa maendeleo ya nchi.

“Nawaombeni mfanye kazi mliyoagizwa mtu aliyekuja akidhani atachukua fedha na kukimbia nimtangazie mapema kabisa atapatikana popote na adhabu yake itakuwa fundisho kwa wengine………tutamtafuta popote alipo na atakua amejiharibia maisha”alisema Mwakyusa.

Awali mratibu wa sensa wilayani humo Monica Sana alisema miongoni mwao watachaguliwa wasimamizi 20 na waliobaki watakuwa makarani na kuwa yeyote atakae onekana hawezi ataondolewa katika mafunzo hayo ili
awekwe mtu mwenye uwezo zaidi.

Blogzamikoa

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa