Home » » NGUZO YA UMEME YATEKETEZA NYUMBA NZIMA

NGUZO YA UMEME YATEKETEZA NYUMBA NZIMA

Na Fadhili Athumani, Moshi
MOTO ulioanzia katika nguzo ya umeme ya Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) umesababisha maafa kwa familia moja, baada ya nyumba yao kushika moto na kutetekea kabisa.

Tukio la kuungua kwa nyumba hiyo lilitokea mjini hapa jana katika Mtaa wa Raha Leo, Kata ya Majengo Manispaa ya Moshi na kusababisha kila kitu kuungulia ndani, baada ya vyombo vya kuzimia moto kuchelewa kufika eneo la tukio.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo akiwamo mtoto wa mwenye nyumba, Kajia Koshuma, aliliambia MTANZANIA kuwa moto huo ulioanzia katika nguzo ya umeme, ulishika nyumba na kisha kusambaa hadi katika vyumba vingine na kuviteketeza kabisa.

“Hadi sasa hatujaweza kujua gharama halisi ya vitu vote vilivyoungua kwa kuwa baadhi ya watu wengi walikuwa sehemu zao za kazi wakati moto huo ukitokea hivyo hatujaweza kuokoa kabisa kitu chochote,” alisema Koshuma.

Kwa upande wao, viongozi wa eneo hilo akiwamo Diwani wa Kata ya Majengo, Peter Minja na Mwenyekiti wa Mtaa huo, Sabitina Mchomvu, waliituhumu TANESCO kwa kuchelewa kufika eneo la tukio kukata umeme uliokuwa katika nguzo hiyo.

“Watu wengi waliowahi kufika eneo la tukio walishindwa kuzima moto huo kutokana na umeme uliokuwapo kuendelea kuwa hai, haukuwa umezimwa hivyo ungeweza kuleta madhara makubwa zaidi kwa watu wengine,” alisema Minja.

Alisema kutokea kwa tukio hilo na uzembe ulioonyeshwa na watendaji wa TANESCO unapaswa kulaaniwa na kuwataka watendaji hao kuwajibika katika nafasi zao za kazi pindi matukio yanapotekea.

Naye, Mwenyekiti wa Mtaa huo, Sabitina Mchomvu, alisema pamoja na madhara yalitokea kusababisha na utendaji kazi wa baadhi ya watendaji, bado ipo haja ya kuhakikisha wananchi wanaanza kujenga nyumba zao kwa kufuata miundombinu itakayorahisha kuokoa maisha ya vitu na watu pindi majanga yanapotokea.

Alisema kufungwa kwa uchochoro uliopo kati ya nyumba hiyo na nyumba za jirani ungesababisha kupunguza kwa uwezekano mkubwa wa kuokoa hata kama gari la kuzima moto lingeweza kufika eneo hilo.

“Ni kweli TANESCO walichelewa kufika lakini pia kitendo cha Mzee Raha Leo kujenga hadi kuziba uchochoro huu na kufunga njia kabisa kumesababisha pia baadhi ya waokoaji kushindwa kunusuru angalau mali kidogo,” alisema Mchomvu.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa