Mwandishi wetu, Rombo-Kilimanjaro Yetu
KUTOKANA na hali ya ukame iliyoukumba mkoa wa Kilimanjaro msimu uliopita, mkuu wa mkoa huo Leonidas Gama amewataka wananchi kununua
chakula na kuhifadhi kipindi hiki ambacho bei ni nzuri ili kukabiliana na upungufu wa chakula.
Gama alisema mkoa unakabiliwa na upungufu mkubwa wa chakula hususan maeneo ya tambarare kutokana na wakulima kutopata mavuno msimu uliopita na kuwataka wananchi wenye uwezo kununua chakula badala ya kusubiri chakula cha msaada kutoka serikalini.
Pia aliwataka wafugaji kupunguza mifugo yao na kununua chakula kipindi hiki ambacho mifugo ina afya ,badala ya kusubiri mifugo kukonda na kukosa bei ndipo wanatafuta soko na kusema kwa msimu ujao serikali
haitaruhusu wakulima kulima mazao ya mahindi maeneo ambayo hayapati mvua za kutosha .
Gama alitoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati wa kikao cha wakuu wa wilaya, wakurugenzi na makatibu tawala wasaidizi kilichokuwa na lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kuinua maendeleo ya mkoa.
Alisema wakulima wengi wamekuwa wakipata hasara kutokana na wao kupanda mazao maeneo ambayo hayana mvua za kutosha na kuwataka kubadilika na kuanza kulima mazao yanayostahimili ukame kama mtama na mbaazi kwani soko la mtama kwa sasa ni kubwa na bei ni nzuri.
Mkuu huyo wa wilaya aliwataka wakulima kuachana na kilimo cha mazoea cha kutumia jembe la mkono na badala yake akawataka waungane kwenye vikundi ili waweze kupatiwa mkopo wa matrekta kutoka Suma JKT ili walime kilimo cha kisasa na chenye tija.
Gama alisema pia kikao hicho kimekaa kujadili maazimio ya kikao walichokaa na Rais Kikwete Dodoma kikihusisha wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya ambacho kililenga kutambua frusa za maendeo zilizopo mkoani na kuona ni zipi zinatoa matokeo ya haraka sanjari na kutambua kipato cha wananchi na kiwango cha umaskini kilichopo.
Akizungumza katika kikao hicho mkurugenzi mtendaji wa manispaa ya Moshi Bernadeta Kinabo alisema kukutana kwao kumeweza kutoa vipaumbele vya kila wilaya na kuwa wao kwa sasa wanaangalia ni jinsi gani ya kufufua viwanda vilivyokufa baada ya kushuka kwa uchumi wa mkoa huo.
Blogzamikoa
0 comments:
Post a Comment