Home » » Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro awapa siku moja wenyeviti wa vitongoji Hai kufafanua wanataka kufanya kazi za serikali ama la

Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro awapa siku moja wenyeviti wa vitongoji Hai kufafanua wanataka kufanya kazi za serikali ama la



 Mkuu wa mkoa wa Kilimanjaro Leonidas Gama akizungumza na wanahabari (pichani chini ) kuhusiana na maandalizi ya Sensa katika mkoa huo.



Na Dixon Busagaga wa 
Globu ya Jamii, Hai.


WENYEVITI wa vitongoji 116 katika wilaya ya Hai,wametishia kutoshiriki zoezi la sensa ya watu na makazi inayotarajia kufanyika usiku wa kuamkia Agosti 26 nchini kote kwa madai wanaidai halmashauri hiyo kiasi cha Sh Mil 280.8 ikiwa ni fedha zao za posho kuanzia mwaka 2009 hadi sasa.



Mkuu wa mkoa huo,Leonidas Gama, aliyasema hayo katika mkutano wake na wanahabari akizungumzia maandalizi ya zoezi hilo ambalo alisema  limekamilika kwa asilimia kubwa .



Pamoja na kuwepo kwa tishio hilo,mkuu wa mkoa alisema wenyeviti hao wamepewa muda wa siku moja kufafanua msimamo wao iwapo wanataka kuendelea kufanya kazi za serikali ama la kutokana na kwamba madai yao

hayahusiani na shughuli ya sensa.



“Kwa sasa tunachangamoto mbili kubwa, hii ya kikundi cha waislamu na hawa wenyeviti wa vitongoji wilayani Hai….nimeongea na viongozi wa wilaya yao nikawataka kama msimamo wao ni kutoshiriki zoezi hili, basi

waandike barua ya kujiondoa katika nafasi zao za uenyekiti”alisema Gama..



Aidha Gama amesema kwa mujibu uongozi wa halmashauri ya wilaya, madai ya wenyeviti hao hayakulipwa mapema kutokana na kukosekana kwa fedha katika bajeti lakini kwa mwaka huu ni miongoni mwa madai yatakayopewa

kipaumbele katika malipo.



Kuhusu kikundi cha waislamu wanaopinga zoezi hilo kilichopo katika wilaya za Same,Mwanga,Moshi mjini na Hai ,Gama alisema tayari jitihada zimefanyika kuwashirikisha viongozi wa madhehebu ya dini ili kuwaelimisha waumini wao kushiriki zoezi hilo.



Alisema mkoa una makarani wa sensa 4937 ambao wamegawanyika katika makundi mawili moja likiwa na makarani 2156 kwa ajili ya kujaza dodoso refu na 2279 kwa ajili ya Dodoso fupi huku makarani wa akiba wakiwa 153 na wasimamizi 349.



Akizungumzia vituo kwa ajili ya zoezi hilo alisema kuna vituo 3357 vilivyogawanywa katika makundi mawili ya Dodoso fupi vilivyopo 2279 na dodoso refu vipo 1078 na kwamba Agosti 23 imetengwa kwa ajili ya kutambua maeneo ya kazi ambapo wataongozwa na wenyeji wao ambao ni wenyeviti wa vitongoji,vijiji na mitaa.



Mkuu wa mkoa aliwataka wananchi kutunza kumbukumbu za taarifa za watu watakaolala katika nyumba zao kwa usiku wa kuamkia Agosti 26 na kwamba zoezi hilo litafanywa kwa siku saba na wasihofu iwapo makarani

hawatafika tarehe 26 bali wasubiri hadi watakapofika kwa takribani siku saba

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa