Home » » RC: WANAOKWAMISHA SENSA WAKAMATWE

RC: WANAOKWAMISHA SENSA WAKAMATWENa Omary Mlekwa, Hai

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, ameagiza hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya watu, taasisi au kikundi cha watu wanaohamasisha mgomo wa Sensa.

Mkuu huyo wa mkoa alisema Sensa haina itikadi za kidini wala za kisiasa na kuwataka waumini wa dini zote kuhesabiwa bila kuweka masharti.

Gama aliziagiza kamati za ulinzi na usalama za wilaya mkoani hapa kuhakikisha vikundi ama viongozi wa taasisi hizo wanakamatwa mara moja na kuwaweka mahabusu, ili wahesabiwe wakiwa huko.

Gama alitoa maagizo hayo katika mikutano yake ya hadhara aliyoifanya katika vijiji vya kata za Rundugai, Masama, Mula na Boma Ng’ombe.

Alisema watu hao watahesabiwa wakiwa mahabusu, kwa kuwa Sensa ipo kisheria na kamwe haina uhusiano wowote na itikadi za kidini wala kisiasa.

Gama alizitaka mamlaka zinazohusika na uratibu wa Sensa ya Watu na Makazi kuhakikisha kuwa changamoto zote zitatuliwe kabla ya tarehe 26 mwezi huu.

Gama aliongozana na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Hai ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya hiyo, Novatus Makunga.

Makunga alisema hadi sasa wilaya yake tayari imeshawatia mbaroni watu saba kwa tuhuma za kuhusika na matukio ya kuhujumu Sensa.

“Kutokana na ukaidi wao sasa watahesabiwa wakiwa mahabusu, kwa kuwa wenyewe walikataa kushiriki Sensa wakiwa uraiani,” alisema Makunga.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa