Home » » WENYEVITI WA VITONGOJI 116 WAGOMEA SENSA

WENYEVITI WA VITONGOJI 116 WAGOMEA SENSA



Na Mwandishi Wetu, Moshi
WENYEVITI wa vitongoji 116 wilayani Hai, mkoani Kilimanjaro, wamegoma kushiriki katika Sensa kutokana na kuidai halmashauri hiyo posho zao katika kipindi cha miaka ninne mfululizo.

Hayo yalibainishwa jana na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusiana na maandalizi ya Sensa.

Gama alisema wenyeviti hao tayari wamekwisha saini barua ya kukataa kushiriki katika Sensa, huku madai yao yakiegemea kutolipwa posho zao kutoka mwaka 2009 mpaka sasa.

Mkuu huyo wa mkoa alisema amewaagiza viongozi wa halmashauri hiyo kuitisha kikao cha dharura na viongozi hao ili kutoa msimamo wao juu ya ushauri wao katika zoezi hilo ili hatua nyingine zifuatwe.

Alisema kukataa kushiriki kwa viongozi hao ni uvunjaji na ukiukwaji wa sheria, kutokana na kwamba kazi hiyo ni ya maendeleo na kwamba madai yao hayana uhusiano na shughuli ya Serikali.

Alisema viongozi hao kugoma kushiriki ni kikwazo kikubwa cha ukamilishaji wa Sensa na kuwataka wenyeviti hao kutambua umuhimu wa kazi hiyo, kwani linawagusa wananchi katika nyanja mbalimbali za maendeleo.

Gama aliongeza kuwa mkoa wake umekumbwa na kundi la baadhi ya watu wanaojiita viongozi wa dini ya Kiislamu, wakishawishi wananchi kutoshiriki Sensa.

Alisema kutokana na hali hiyo, ameziagiza Kamati ya Ulinzi na Usalama kuweka ulinzi wa kutosha katika kipindi hicho ili kukabiliana na wimbi la watu hao.

Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa