Home » » WAHAMIAJI HARAMU 39 WANUSURIKA KUFA

WAHAMIAJI HARAMU 39 WANUSURIKA KUFA

Na Upendo Mosha, Moshi
WAHAMIAJI haramu 39, wamenusurika kifo baada ya gari walilokuwa wakisafiria kugonga kingo za daraja la Mto Ghona, wilayani Moshi, kisha kuacha njia na kupinduka.

Katika ajali hiyo, wahamiaji 27 walijeruhiwa vibaya ambapo mmoja kati yao, amelazwa katika chumba cha wagonjwa mahututi (ICU).

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini wake jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz, alikiri kutokea kwa tukio hilo.

Alisema tukio hilo lilitokea jana mchana katika eneo la Mambungo, barabara ya Moshi-Himo.

Alisema baada ya kupatikana taarifa za kuwepo wahamiaji hao, polisi walifika eneo hilo la tukio na kukuta gari lenye nambari za usajili T 958 ARB ana ya Mitsubishi Canter.

Alisema polisi waliamua kulikagua na kubaini ndani kulikuwa na wahamiaji haramu 39 na kuamua kulipeleka gari hilo katika Kituo cha Polisi Himo.

Alisema wakati gari hilo likiwa njiani kuelekea kituoni, lilipokaribia daraja la Mto Ghona likiwa mwendo kasi liligonga kingo za mto huo, kisha kuacha njia na kupinduka.

“Leo (jana) saa 6 mchana, tulipokea taarifa kuwa kuna wahamiaji haramu 39, kati yao watano ni Wasomali wengine ni Waethiopia, wakati wanapelekwa kituoni gari lao lilipata ajali na kupinduka,” alisema Boaz

Alisema mmiliki wa gari hilo, ndiye dereva aliyekuwa akiendesha gari hilo, John Peter Omar.

Wahamiaji hao, wamelazwa katika Hosptali ya Rufaa ya KCMC wakiendelea kupata matibabu.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa