na Rodrick Mushi, Moshi
WANANCHI wa Kijiji cha Mdawi, Kata ya Kimochi, Wilaya ya Moshi Vijijini, wamemlalamikia Mtendaji wa kijiji hicho, Lenard Mende kushindwa kuwepo ofisi siku za kazi pamoja na kutohudhuria mikutano ya serikali inayojadili shughuli za maendeleo ya kijiji.
Wakizungumza baada ya kufunguliwa kwa mkutano huo na kuahirishwa bila kujadili agenda yoyote, baadhi ya wananchi hao walisema kuwa, hiyo ni mara ya pili kushindwa kufanyika kwa mkutano huo kutokana na mtendaji huyo kutokuwepo.
Mwenyekiti wa kijiji hicho, Rumisha Kinyaa, aliwaeleza wananchi waliokuwa wamefika kwenye mkutano huo kuwa walikuwa wamempa mtendaji taarifa ya uwepo wa mkutano huo, lakini hakufika.
Alisema kuwa, hawatandelea na mkutano huo, ilihali mwakilishi wa Mkurugenzi hayupo, hivyo agenda mbalimbali ambazo zingejadiliwa kwa siku hiyo, ingekuwa ni kazi bure kama wangefanya bila uwepo wa mtendaji.
“Miongoni mwa mambo ambayo wananchi walikuwa wahoji kwenye mkutano huu, ni pamoja na kutokufika kwa mtendaji huyu ofisini siku za kazi, jambo ambalo limekuwa kero kubwa kwetu, wakati yeye ameletwa kwa ajili ya kushirikiana na sisi kuleta maendeleo,” alisema Kinyaa.
Naye Diwani wa Kata ya Kimochi, Anamenyisa Macha, alisema kuwa changamoto nyingi zinazotokea kwenye Kijiji hicho zinatokana na itikadi za kisiasa ambazo zinasababishwa na mvutano wa vyama pamoja na wananchi kupingana na kugawiwa kwa kijiji cha Mdawi.
Alisema kuwa, kinachotakiwa ni wananchi na viongozi kuondoa itikadi zao na kuwatumikia ili kuweza kuleta maendeleo, pamoja na kuchunguza malalamiko yaliyopo kwamba hawakushirikishwa katika ugawaji wa kijiji hicho.
Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Ibrahim Msengi, alipuulizwa kuhusiana na tatizo lililopo kwenye kijiji hicho, alisema kuwa amebanwa na shughuli za mbio za Mwenge ambao ulikua mkoani Kilimanjaro, huku akiahidi kulifuatilia baada ya kumalizika kwa mbio hizo.
Naye Mtendaji wa Kijiji anayelalamikiwa, alipopigiwa simu, alidai kuwa yupo kwenye eneo lenye kelele, hivyo hataweza kusikilizana na mwandishi na alipotafutwa baadaye simu yake haikupatikana tena.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment