Home » » CHADEMA YAMJIBU JUU RC

CHADEMA YAMJIBU JUU RC

na Rodrick Mushi, Moshi
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Manispaa ya Moshi kimemjia juu Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, kuhusiana na taarifa aliyotoa juu ya safari ya madiwani hao kwenda Rwanda na kusema anatumika kisiasa na Chama cha Mapinduzi (CCM) kwa lengo la kuwagombanisha madiwani hao na wananchi.
Wakizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Mji Mpya uliohudhuriwa pia na aliyekuwa Mbunge wa Arusha, Godbless Lema, CHADEMA kilisema kama Mkuu huyo wa Mkoa akiendelea kutumika kisiasa na kuacha shughuli za utendaji wa kuwatumikia wananchi, watatangaza mgogoro naye wa kutoshirikiana kwenye shughuli zozote.
Akizungumza kwenye mkutano huo, Meya wa Manispaa ya Moshi, Japhary Michael, alisema safari ya madiwani hao ni stahili yaliyopo kisheria kwenye miongozo ya nchi, hivyo mkuu huyo wa mkoa hana mamlaka ya kuyazuia na kama CHADEMA walikuwa wana malengo mabaya, wasingewashirikisha Waziri Mkuu na Mkuu wa Mkoa ambao ni viongozi kutoka CCM.
“Mafunzo ya madiwani na watendaji hayakupangwa na CHADEMA, au Mwenyekiti, Freeman Mbowe. Mafunzo hayo ni kwa halmashauri zote nchini ni kwanini wakuu wengine wasizuie?” alihoji meya.
Japhary alisema, kwa muda ambao amekuwa meya amepokea zaidi ya halmashauri 20 kutoka sehemu mbalimbali ambao wamekuwa wakija kwenye Manispaa ya Moshi kujifunza usafi wa manispaa hiyo na wanakwenda kwa muongozo wa taifa ambao unaelekeza lazima madiwani wapate mafunzo.
Akielezea safari ya Rwanda iliyogharimu sh. milioni 123.2, alisema ilikuwa na lengo la kujifunza zaidi jinsi ya kuufanya Mji wa Moshi kuendelea kuwa msafi.
Diwani wa Kata ya Longuo B, Reymond Mboya, alisema mkuu huyo wa mkoa alidanganya wananchi kuwa bajeti ya Manispaa mwaka jana ilikuwa na upunguafu wa asilimia 40, kitu ambacho si kweli, kwani bajeti hiyo ilikuwa ina upungufu wa asilimia 8.19.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa