Home » » DC HAI AWASIMAMISHA VIONGOZI WA KIJIJI KWA UBADHIRIFU

DC HAI AWASIMAMISHA VIONGOZI WA KIJIJI KWA UBADHIRIFU

Na Omary Mlekwa, Hai
MKUU wa Wilaya ya Hai, Novatus Makunga, amewasimamisha uongozi Mwenyekiti wa Kijiji cha Kwasadala, Ernest Munisi na Ofisa Mtendaji wake, Clare Ramadhani kwa ajili ya kupisha uchunguzi wa tuhuma za ubadhirifu wa mali za kijiji na uuzaji holela wa maeneo ya wazi.

Uamuzi huo aliutangaza katika mkutano wa hadhara wa kijiji hicho ambapo aliagiza viongozi hao kukaa pembeni kupisha uchunguzi huo utakaofanyika katika kipindi cha wiki moja kuanzia Jumatatu ijayo.

Alisema uchunguzi huo utafanywa na timu ya wataalamu watano kutoka katika Halmashauri ya Wilaya ya Hai.

Aliwataja wataalamu hao kuwa ni mwanasheria, mkaguzi wa ndani, ofisa ardhi, ofisa utumishi na ofisa ugavi pamoja na katibu tawala wa wilaya.

Alisema matokeo ya uchunguzi huo yatatoa mwelekeo wa hatua za kuchukuliwa.

Katika mkutano huo, wananchi mbalimbali walitoa tuhuma dhidi ya mwenyekiti wa kijiji hicho kuuza holela maeneo ya ardhi na fedha kuzitumia kwa matumizi binafsi.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi wa kijiji hicho walijitokeza na kumtetea mwenyekiti huyo kwa madai ya kuleta maendeleo makubwa yakiwamo ya ujenzi wa shule ya msingi na Sekondari ya Mkwassa na kudhibiti wimbi la ujambazi

Mwananchi wa Kijiji hicho, Judica Swai, alisema maeneo ya wazi ya kijiji hicho yakiwamo ya Shule ya Msingi ya Msamadi yamekuwa yakiuzwa holela na uongozi wa kijiji hicho na kila aliyejaribu kuhoji amekuwa akifanyiwa visa vikiwamo vya kufunguliwa kesi za kubambikiwa.

Naye, David Swai, aliutuhumu uongozi huo kuuza mizani ya kupimia mazao ya kijiji hicho pamoja na uongozi wa kijiji kwa zaidi ya miaka miwili sasa na kushindwa kusoma taarifa za mapato na matumizi kutokana na kutofanyika kwa mikutano.

Walisema maeneo ya ardhi ya kijiji hicho yamekuwa yakiuzwa bila ya kufahamika fedha zinaenda wapi pamoja na kutokuwapo kwa taarifa ya michango inayokusanywa kutoka kwa wananchi.

Walidai mwenyekiti huyo amesababisha migogoro mikubwa ukiwamo baina ya kijiji na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kuhusiana na mvutano wa ardhi ambapo mgogoro huo kwa sasa upo mahakamani.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa