na Charles Ndagulla, Moshi
MAOFISA
wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika kituo cha Forodha cha Holili
wameingia katika kashfa wakihusishwa na upokeaji rushwa ya mamilioni ya
fedha kutoka kwa wafanyabiashara wanaojihusisha na usafirishaji wa
sukari kwenda nchini Kenya kwa njia za magendo.
Uchunguzi
uliofanywa na Tanzania Daima Jumatano umefichua mipango yote
inayofanywa na maofisa hao wakishirikiana na wafanyabiashara wa magendo
ya sukari kuikosesha serikali mamilioni ya fedha.
Gazeti
hili katika uchunguzi wake limebaini kuwa kabla ya wafanyabiashara hao
kuvusha shehena ya sukari kwenda nchini Kenya ambako inaaminika
kumekuwapo na uhaba wa sukari, hufanya vikao vya kuweka makubaliano ya
kiwango cha rushwa kitakachotolewa na wafanyabiashara hao.
Inadaiwa
kila gari moja aina ya Fuso Tandamu maofisa hao wenye dhamana ya
kukusanya kodi kwa niaba ya serikali, hupokea wastani wa sh 300,000 na
500,000 kulingana na makubalino baina ya mfanyabiashara anayesafirisha
sukari.
Kwa
muda wa wiki moja sasa wastani wa magari 10 hadi 15 yamekuwa
yakisafirisha sukari kila siku kutoka mji mdogo wa Himo kwenda nchini
Kenya kupitia njia ya kwa Mandara hadi eneo kunakochimbwa mchanga aina
ya Pozolana wilayani Rombo kabla ya kuingia nchini Kenya kupitia njia za
panya.
Kazi
hiyo ya kusafirisha sukari kwenda nchini Kenya kwa njia za magendo
hufanikishwa na askari mgambo waliopo eneo la kwa Hussen nje kidogo ya
mji mdogo wa Himo ambapo jukumu lao ni kuhakikisha wanasindikiza magendo
hayo hadi mpakani mwa Kenya na Tanzania.
Mmoja
wa mgambo hao aliyeomba jina lake lisitajwe kwa hofu ya kupoteza
kibarua chake, alimeliambia Tanzania Daima Jumatano kuwa wamekuwa
wakilipwa ujira wa kati ya sh 30,000 hadi sh 50,000 kwa kusindikiza
magari yaliyosheheni sukari.
Kwa
mujibu wa uchunguzi wetu biashara hiyo ya magendo ya sukari
imewawezesha mgambo wengi katika ukanda huo wa Holili na Himo kuwa na
kipato kikubwa huku baadhi yao wakifanikiwa kujenga nyumba za kisasa
pamoja na kununua magari ya aina mbalimbali.
Wengine
ambao wamekuwa wakinufaika na biashara hiyo ya magendo ya sukari ni
askari wa kituo cha polisi Himo ambao hupokea rushwa ya wastani wa sh
500,000 hadi 700,000 kwa kila gari, rushwa ambayo imepewa jina la
‘safisha njia’.
Uchunguzi
umebaini kuwa askari hao pamoja na maofisa wa TRA, huyaondoa magari yao
ya doria kwenye barabara ambazo hutumika siku ya kusafirishwa kwa
sukari hiyo na kwenda kupiga doria eneo jingine lengo likiwa ni kuruhusu
shehena za sukari kupita bila woga.
Hata
hivyo, meneja wa TRA mkoani Kilimanjaro, Patience Minga, hakuwa tayari
kujibu ujumbe mfupi wa maandishi aliotumiwa na mwandishi wa habari hizo
kutaka ufafanuzi juu ya tuhuma zinazowakabili maofisa wake.
Pamoja
na mwandishi kutuma ujumbe mfupi wa maandishi kupitia simu ya
kiganjani, jana pia hakuwa tayari kupokea simu ya mwandishi wa habari
hizi na kila ilipopigwa iliita bila kupokelewa.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment