na Rodrick Mushi, Moshi
CHAMA Kikuu cha Ushirika mkoani Kilimanjaro (KNCU) kimemtaka Mbunge wa Vunjo, Augustino Mrema (TLP), kufuta kauli kuwa viongozi wa chama hicho ni majambazi na wamekuwa wakiwaibia wakulima kwenye bei ya kununua zao la kahawa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Mwenyekiti wa KNCU, Mynard Swali, alisema endapo Mrema hatafuta kauli hiyo watamburuza mahakamani ili kurudisha heshima ya chama hicho.
Swai alisema alipata simu kutoka kwa Mrema akitaka KNCU kuhudhuria kwenye vikao ambavyo angefanya na vyama vinane vilivyopo jimbo la Vunjo, lakini chama hicho kilimjibu kutohudhuria kutokana na kutokuwepo kwa taratibu nzuri za maandalizi ya vikao pamoja na kutojua agenda yake.
Alisema licha ya KNCU kutomkubalia Mrema, aliamua kuwadanganya wananchi kupitia barua aliyoandika Agosti 23 kuwa ataongozana na wataalamu wa KNCU kwenye ziara yake na kutangazwa kwenye nyumba za ibada.
“Tunazungumza haya si kwa lengo la kuleta malumbano, hapana, sisi sio wanasiasa, anachotaka kufanya Mrema ni kuvuruga amani, kwani taarifa ambazo alitoa kwenye vikao hazina tija bali zinataka kuondoa imani kati ya KNCU na wanachama wake,” alisema Swai.
Kuhusu bei ya kununulia zao la kahawa, Swai alisema chama hicho hakihusiki kupanga bei.
“Chama cha ushirika hatujamuomba Mrema kuwa msemaji, tungefurahi kama angeungana na sisi katika kudai fedha sh Mil. 255 ambazo serikali ilikuwa imeahidi kuwa ingezitoa kwa chama baada ya mdororo wa uchumi duniani, lakini sio kuwadanganya wananchi waandamane,” alisema.
Hata hivyo, Mrema alisema hajawatukana viongozi hao na hawezi kufanya hivyo na kama KNCU wameamua kusema hivyo, watakuwa ni waongo.
“Mimi siyo mjinga kiasi hicho mpaka niende nikawatukane viongozi hao kuwa ni majambazi, kwani wameiba nini?” alihoji Mrema.
Chanzo: Tanzania Daima
0 comments:
Post a Comment