Home » » WENYEVITI WA VITONGOJI WAILAYA YA HAI WASEMA ‘DC HANA MAMLAKA KUTUFUKUZA KAZI’

WENYEVITI WA VITONGOJI WAILAYA YA HAI WASEMA ‘DC HANA MAMLAKA KUTUFUKUZA KAZI’

na Rodrick Mushi, Hai
UMOJA wa Wenyeviti wa Vitongoji wilayani Hai, umesema mkuu wa wilaya (DC) hana mamlaka ya kuwafukuza kazi na kuongeza kuwa, Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama, alitoa kauli hiyo kisiasa.
Gama alitoa kauli hiyo siku moja baada ya watendaji hao kususia kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa hadi watakapolipwa malimbikizo ya posho ya zaidi ya sh milioni 280.
Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Simon Mnyampanda, alitoa kauli hiyo jana alipokuwa akimtaka Gama kufuta kauli ya kumtaka Mkuu wa Wilaya hiyo, Novatus Makunga, kuwafukuza kazi watendaji hao.
“Suala hili mkuu wa mkoa alilizungumza kisiasa, na kutokana na nafasi aliyonayo, lakini ukweli ni kwamba sheria zinaonyesha hana mamlaka ya kutufukuza, sisi hatuwajibiki kwake, tunawajibika kwa wananchi,” alisema Mnyampanda.
Alisema kwenye kikao walichokaa na Makunga walikubaliana kutoa ushirikiano kwa makarani wa sensa, lakini kuendelea na mgomo wao wa kutowajibika kwa shughuli zozote za maendeleo hadi watakapolipwa madai yao.
Akichangia, mmoja wa wenyeviti wa vitongoji, Godluck Munisi, alisema wananchi hawana imani na serikali yao, kwani watendaji hao ambao ni nguzo muhimu kwenye uongozi wa nchi, wamekuwa wakizungushwa kwenye kulipwa haki yao.
Chanzo: Tanzania Daima

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa