na Rodrick Mushi, Moshi
MTOTO wa Baba
wa Taifa, Madaraka Nyerere, ameshauri mfumo wa elimu nchini kufanyiwa
marekebisho vinginevyo taifa litaendelea kuwa na wasomi wasiokuwa na sifa.
Amesema mfumo
wa elimu unatakiwa kuangaliwa upya kuanzia elimu ya msingi hadi vyuo, ili taifa
liweze kuzalisha wahitimu wenye elimu bora.
Madaraka alitoa
kauli hiyo mwishoni mwa wiki kwenye mahafali ya sita ya kidato cha nne ya Shule
ya Sekondari Sungu iliyoko wilaya ya Moshi Vijijini, mkoani Kilimanjaro.
Alisema kama
serikali inavyoita ukimwi kuwa ni janga la taifa, hata sekta ya elimu imegeuka
janga la taifa na kwamba inahitaji kufanyiwa maboresho na mapambano ikiwa ni
pamoja na kutenga bajeti ya kutosha.
“Kumaliza
tatizo la elimu sio suluhisho la muda mfupi, kwani inatakiwa kufumuliwa kabisa
kwa mfumo mzima wa elimu na kuhakikisha wanafunzi wanakuwa na sifa kwa sababu
unaweza kukutana na mhitimu wa Chuo Kikuu mpaka unajiuliza amehitimu namna gani
elimu hiyo kwani unakuta hana sifa,” alisema.
Kwa upande
wake, mkuu wa shule hiyo, James Thomas, alisema wananchi wa eneo hilo wamekuwa
wakitoa ushirikiano mkubwa kwenye suala la kuchangia elimu na ndiyo maana shule
hiyo imekuwa na maendeleo mazuri.
Pamoja na hayo,
alisema shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ukosefu wa
maabara, maktaba pamoja na bwalo la kulia chakula kwa wanafunzi.
Chanzo: Tanania Daima
0 comments:
Post a Comment