Home » » MGOGORO WAKWAMISHA KIKAO CHA MADIWANI

MGOGORO WAKWAMISHA KIKAO CHA MADIWANI



na Rodrick Mushi, Hai
MBUNGE wa Jimbo la Hai, Freeman Mbowe, amesema kutofuatwa kwa Kanuni za Halmashauri zinazoelekeza taratibu za uitishwaji wa vikao kumechangia kutofanyika kwa Kikao cha Baraza Madiwani, Septemba 24, mwaka huu.
Akizungumza baada ya kuairishwa kwa kikao hicho, Mbowe alisema mgogoro uliopo baina ya Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Melkizedeki Humbe na Mwenyekiti wa baraza hilo, Clement Kwayu (CHADEMA), unasababishwa na Humbe kutofuata kanuni na kutomshirikisha Kwayu.
Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, alisema kikao hicho ni cha mwaka na kilikuwa kijadili taarifa ya maendeleo, kumchagua Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo na viongozi wa kamati mbalimbali.
Mbowe alisema, mgogoro uliokuwepo usingestahili kuwepo kwani tofauti zinazotokana na mkurugenzi kuitisha vikao bila kushirikisha mamlaka ya mwenyekiti ambae ndiye anayesimamia vikao vya halmashauri.
“Wakurugenzi wasimamie halmashauri kwa kanuni na kwa mujibu wa sheria na miongozi iliyopo na si kufuata maagizo ya wakuu wa mikoa, wilaya au wabunge,” alisema Mbowe.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Humbe alisema kikao hicho kimeshindwa kufanyika baada ya kushindwa kufikia ahadi kulingana na kanuni za uendeshaji wa vikao vya baraza.
Alisema mvutano huo ni wa kisiasa, huku akikiri kupata barua kutoka kwa madiwani wa CCM wakitaka msuluhishi kutoka ngazi ya mkoa baada ya kuairishwa kwa kikao cha kwanza kilichokuwa kikae Agosti 30 ambacho madiwani wa CHADEMA walishindwa kufika kwa sababu ya zoezi la sensa lililokuwa likiendelea.
Humbe alisema kikao hicho kilikuwa muhimu kwani kilikuwa pia kikichagua viongozi wa kamati mbalimbali ikiwamo ujenzi, uchumi na mazingira.
Chanzo: Tanzania Daima


0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa