Home » » WANAFUNZI WALIOFUTIWA MITIHANI WAPEWA NAFASI NYINGINE

WANAFUNZI WALIOFUTIWA MITIHANI WAPEWA NAFASI NYINGINE

Na Omary Mlekwa, Hai
MWENYEKITI wa Kamati ya Usimamizi wa Mitihani Mkoa wa Kilimanjaro, Ruth Malisa, amewataka wanafunzi 147 waliofutiwa mtihani wa kumaliza elimu ya sekondari mwaka jana kutoka wilayani Hai, kutoichezea fursa waliyopewa ya kuruhusiwa kufanya tena mtihani huo.

Aliwataka wasimamizi wa mitihani wilayani Hai kutambua michango wa idadi ya waliofutiwa mtihani katika mkoa wa Kilimanjaro kwa mwaka jana ilikuwa kubwa, kwa kuwa mkoa wote ulikuwa na wanafunzi waliofutiwa mtihani wapatao 530.

Malisa, ambaye pia ni Katibu Tawala wa Mkoa Msaidizi anayehusika na elimu, amewataka walimu hao kuhakikisha wanazipitia na kuzielewa taratibu zote za usimamizi wa mitihani, kwa kuwa dosari zozote zitakazojitokeza katika vyumba vya mitihani watakaowajibika ni wao.

Aliwakumbusha kuhakikisha madawati yote yenye maandishi na ukuta unafutwa, huku ramani zikiwa zimefunikwa na umbali kati ya dawati na dawati la mtahiniwa kuwa mita moja, huku mkondo mmoja wa darasa la watahiniwa lisizidi watahiniwa 25.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Mitihani wilayani Hai, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Hai, Melkizedeck Humbe, alisema uteuzi wa wasimamizi hao ulizingatia maadili kwa ajili ya kuhakikisha tatizo la udanganyifu halijitokezi tena.
Chanzo: Mtanzania

0 comments:

 
Supported by Tone Multimedia Company Limited
Copyright © 2012. Kilimanjaro Yetu - All Rights Reserved
Designed by Fredy Tony Njeje
Proudly powered by Blogs za Mikoa